GHARAMA
za
kupiga simu kutoka mtandao wa kampuni moja ya simu za mikononi kwenda mwingine
nchini kuanzia Machi Mosi, mwaka huu, zitashuka kutoka Sh. 115 hadi Sh. 34.92
kwa dakika moja.
Uamuzi huo umefanywa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) baada ya kufanya
mapitio ya gharama za mwingiliano kwa kampuni za simu nchini wa mwaka 2013, pia
kuanzia Januari Mosi, mwakani, gharama hizo zitapungua hadi Sh. 32.40.
Vilevile, Januari, 2015 gharama hizo zitashuka hadi Sh. 30.58; Januari, 2016
zitashuka hadi Sh. 28.57 na Januari, 2017 zitashuka hadi Sh. 26.96 kwa dakika
moja. Akitangaza uamuzi huo jijini Dar es Salaam jana, Mkurugenzi Mkuu wa
TCRA, Profesa John Nkoma pichani, alisema umetolewa kwa mujibu wa sheria ya TCRA ya
mwaka 2003 Sura 172.
Profesa Nkoma alisema viwango hivyo ni vya kikomo cha juu na pia ni elekezi,
lakini akasema kampuni za simu zina uhuru wa kukubaliana kibiashara ili mradi
makubaliano yao yasizidi gharama zilizoelekezwa na TCRA. Alisema gharama hizo
zitatumika kwa mawasiliano ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na simu za
kimataifa zinazoingia katika mitandao nchini.
Hivyo, ameziagiza kampuni zote za simu kufanya makubaliano mapya baina yao na
kuwasilisha nakala ya makubaliano kwa TCRA ifikapo Machi 31, mwaka huu. Alisema
gharama hizo zimeshushwa ili kuwafanya watumiaji wa simu kuwa huru kupiga simu kwenda
mtandao wa kampuni yoyote ya simu na kuwaondolea mzigo wa kubeba ‘laini’ nyingi
za mitandao tofauti ya simu kwa wakati mmoja.
Pia alisema ana imani kuwa uchangiaji wa matumizi ya miundombinu na matumizi ya
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (Ucaf) na mkongo wa taifa wa mawasiliano, ndiyo
suluhisho la kushuka kwa gharama za uendeshaji na kuenea kwa mawasiliano
vijijini.
Alisema watumiaji wa simu za mikononi wamekuwa wakilazimika kubeba ‘laini’ za
mitandao tofauti, ambazo kila moja huitumia kupiga simu kwenda kwenye mtandao
unaofanana nayo.
Profesa Nkoma alisema wamekuwa wakifanya hivyo ili kukwepa kutozwa
gharama kubwa za kupiga simu kutoka mtandao mmoja wa simu za mikononi kwenda
mwingine.
Alisema uamuzi wa kushusha gharama za mwingiliano wa mawasiliano ya simu
za mikononi utakuwa sheria, ambayo kampuni zote za simu zitalazimika kutii.
“Sasa hivi tuna mitandao kama saba ya simu. Ni bughudha kwa wananchi
kutembea na mzigo wa ‘sim card’ (‘laini’) ili kukwepa gharama za kupiga simu
kutoka mtandao mmoja kwenda mwingine,” alisema Profesa Nkoma na kuongeza:
“Sisi kama mdhibiti tunaona hali hii si nzuri. Tunataka mtu awe huru
kupiga simu mtandao wowote.” Hata hivyo, alisema kama itatokea sababu ya
bei hizo kuangaliwa upya, TCRA itafanya hivyo. Alisema suala la kushuka
kwa gharama za mwingiliano wa mawasiliano ya simu kutoka mtandao wa kampuni
moja kwenda mwingine, hivi sasa linatumika duniani kote, zikiwamo nchi jirani,
kama vile Kenya, Uganda na Rwanda. Nipashe.
No comments:
Post a Comment