1. Acha kukuna makovu ya mende (Kichaga)
Maana yake ni kwamba uache kukumbuka taabu ya wakati uliopita. Methali hii itafahamika vizuri kama tukielewa kwamba hapo zamani katika jamii zetu, mende walikuwa wanaonekana kwa wingi katika nyumba. Nao mende ni hodari wa kuuma watu wakati wa usiku wakiwa wamelala. Na pale walipouma hubaki kovu ambalo hukuna. Lakini pia ambaye ameshaumwa na mende hao itakuwa ni kazi bure kama atakalia kuyakuna makovu hayo.
Methali hii hutumika kwa kuwaonya watu wasikalie kufikiria makosa au taabu za wakati uliopita.
2. Afadhali kuchakaza nguo kuliko akili (Kipare)
Maana yake ni kuwa hakuna kitu bora kama akili (hekima). Mtu ambaye hana hekima ya uchi kuliko uchi wa aina yoyote ile. Kuwa uchi kinguo, mtu anaweza kununua zingine. Lakini mtu anapokuwa uchi kiakili, hakuna maarifa.
Methali hii hutumika kwa kumhurumia mtu ambaye ameharibikiwa na akili na anafanya majambo isivyotakiwa katika jamii.
3. Amekufa hata Mwakafwile aliacha mwana alipokufa (Kinyakyusa)
Methali hii inatokana na mila za kibantu kukosa mrithi ni mwisho wa ukoo na jina la ukoo. Mtoto wa kiume huendeleza ukoo. Ni jambo la kusikitisha sana kutokuwa na mwana mrithi.
Maana ya methali hii ni kwamba mtu anayehusika hana msaada wowote kutoka kwa ndugu, jirani au mahali penginepo.
Hutumika na mtu binafsi aliyezama ndani ya kilindi kikubwa cha matatizo, wala hana mtoto au mtu wa karibu naye ambaye angeweza kumsaidia. Ni methali ya watu maskini na wanyonge katika kuhurumiana shidani. Kama kuunguliwa nyumba, kufiwa nk.
4. Anayetaka usawa mwisho wake uchawi (Kikerewe)
Methali hii ina maana kwamba tukubali kuwa binadamu budi kutofautiana. Fulani kapata baiskeli – lazima nami nipate, fulani kapata nyumba – lazima nami nipate nk. Maneno kama haya mwishowe humsukuma mtu kutumia hila mbaya au njia zisizo za kawaida kama vile uchawi.
Methali hii hutumika katika kuwaonya wanopenda kujikweza.
5.Fimbo ya jirani haiui nyoka (Kiiraqw)
Ujirani ni jambo jema lakini si vizuri kutegemea misaada yote toka kwa majirani. Methali hii inafundisha umuhimu wa kujitegemea na si kutazamia kupata misaada kila uhitajipo.Pia, ni lazima ieleweke kwamba hakuna sheria inayomfanya jirani atoe msaada hata kama anaweza, yote hutegemea matakwa yake na huwezi kubashiri ni lini atakataa kutoa msaada.
6. Fungo alikosa mkia kwa kulala (Kizigua na kinguu)
Ipo hadithi katika hadithi za Kizigua na Kinguu isemayo kuwa kwa sababu ya usingizi wake Fungo alikosa au aliupoteza mkia wake. Methali hii inaonyesha hasara ya uzembe na kuchelewa mara nyingi. Hali hii inaweza kumkosesha mtu mambo mengi mazuri au kupoteza maslahi yake ambayo yangemfaa baadaye. Hutumika kama onyo kwa wazembe.
7. Anayelala na mgonjwa ndiye anayejua miugulio (Kisambaa)
Maana yake ni kwamba huwezi kujua undani wa mtu mpaka uwe naye karibu katika uhusiano. Hutumika kwa mtu anayejitia kujua sana mambo ya ndani ya wengine kuliko wenyewe wanaohusika.
8. Hohehahe hakosi siku yake (Kiha)
Maana yake ni kuwa kila mtu ana bahati yake. Hata maskini ana siku yake ya bahati. Hutumika kama onyo kuwa inafaa kuthamini watu kwa utu wao na wala si kwa mali walizonazo. Mtu ni utu.
9. Kondoo wa madoadoa hawako katika jamii ya wanadamu (Kimasai)
Wanadamu wote hawahitilafiani sana kwa maumbile yao, na ndio maana tunaweza kusema, binadamu wote ni sawa. Tusikiapo kitu kisicho cha kawaida kuhusu mtu tunaweza kutumia msemo huu kumaanisha kwamba tumestaajabishwa na habari hizo. Msemo huu unatumika pia katika kukanusha habari zisizoaminika.
10. Kucheka chongo ya mwenzio na hali yako umefunika (Kisukuma)
Maana yake ni kuwa si vizuri kucheka makosa ya wengine kwani huenda ukafanya makosa yale yale na pengine una udhaifu wako ambao wengine wanakucheka. Hutumika katika kuwaonya watu wanaocheka dosari au udhaifu wa watu wengine na pengine watu wanaocheka wenzao waliopatwa na maafa k.m. kufilisika.
11. Mbwa mwenye mnofu mdomoni hapigi kelele (Kifipa) Maana yake ni kama methali ya kiswahili isemayo:- Mwenye shibe hamjui mwenye njaa. Methali hii hutumiwa kwa kuwasema watu ambao wana kitu na huwasahau wale ambao hawana kitu. Zaidi, huweza kutumika kwa kuwaonya viongozi wanaosahau kuwatetea wenzao baada ya kupata madaraka na shibe.
12. Mwenda usiku amesifiwa kulipokucha (Kikwere) Mwenda usiku hapa ni sawa na mtu ayetenda jambo ambalo kwa wakati ule wengine hawalielewi. Lakini mwishowe jambo hilo lilipoonyesha mafanikio ndipo watu wakaanza kumsifu. Hutumika kwa mtu anayechekwa na wenziwe juu ya jambo alitendalo iwapo wakati ule wale wamchekeo hawaelewi usahihi wa lile alitendalo.
13. Nguo ya mzee haikosi chawa (kimeru) Maana yake, mzee hakosi akiba. Maana ya methali hii itafahamika zaidi si kwa vile hali ya uchafu ndiyo iletayo chawa, bali kwamba kwa mzee huwa na akiba za aina aina nayo maana yake ni ile nzuri. Methali hii hutumika wakati mtu anapozungumzia utajiri wa mtu mzee. Ni kama njia ya kuwakoga wengine kwamba wakati wote utazamie kumkuta mzee katka hali nzuri, anayo akiba yake ambayo ameihifadhi.
14. Usidharau wakunga uzazi ungalipo (Kibena) Wakunga ni watu wenye kuheshimiwa sana kwa sababu ya ufundi na ujuzi wao wakati wa kuzalisha. Kwa kuchukua umuhimu wao huo, wanawake hushauriwa kutowadharau maadamu wangali wanazaa, isijeikawa wakti wa kujifungua wakakosa msaada. Matumizi ya methali hii ni kuwaonya watu kwa ujumla wasiwe na dharau kwa kitu ambacho kitawafaa katika maisha yao. Zaidi kwamba, kitu kilichokusaidi wakati uliopita usikidharau kwa vile hukitumii kwa wakati huu.
No comments:
Post a Comment