Prof. Aldin K. Mutembei
Taasisi ya Taaluma za Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Wakati huo huo, Chama cha Kiswahili cha Taifa, Kenya – CHAKITA kiliandaa mkutano Jijini Nairobi wa kukumbuka miaka 50 ya Kiswahili nchini Kenya. Mkutano huo pia ulifanyika tarehe 20 hadi 24 Agosti, 2013. Kwa hiyo, Jarida la HABARI kuamua kujadili kuhusu fasihi ya Kiswahili nchini Tanzania, limekuwa ni jambo jema na linaloendana na matukio yanayohusu mwamko wa Kiswahili Tanzania na Afrika mashariki kwa ujumla. Mwamko ambao sasa umo zaidi miongoni mwa vijana wa sekondari na wale wa vyuoni. Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili wa Vyuo Vikuu vya Afrika mashariki - CHAWAKAMA kitawakutanisha wanafunzi kuendeleza mjadala kuhusu Kiswahili nchini Rwanda na Afrika mashairiki kwa ujumla mwishoni wa Agosti 2013. Basi, Jarida la HABARI kweli linaleta habari na taarifa ambazo zinakwenda na wakati na mambo yalivyo uwandani Afrika mashariki.
Katika makala hii fupi, nitajadili kwa ujumla, hali na maendeleo ya fasihi. Sitaangalia mawazo kuwa kuna fasihi miongoni mwa Waafrika au la. Mabishano hayo yamekwisha kuangaliwa mahali pengine hasa tangu miaka ya 1970, na kutokeza vitabu viwili muhimu katika mjadala huo: kile cha Ruth Finnegan (1970) na baadaye kile cha Isidore Okpewho (1992) kuhusu fasihi katika Afrika na fasihi ya Kiafrika. Fasihi ya Kiafrika bado inaendelea kupata mengi kutoka katika masimulizi, na utafiti mwingi hauna budi kufanyika kuhusu yale ambayo hayajaandikwa na wala hayafahamiki miongoni mwa wale ambao hasa hupata maarifa kutoka katika maandishi. Fasihi ya Afrika ni utanzu uliokomaa sasa na kujipambanua miongoni mwa fasihi za ulimwengu.
Hata hivyo, makala hii itaangalia hali ya fasihi ya Kiswahili nchini Tanzania katika miaka ya sasa. Tutaangalia kuibuka kwa tanzu simulizi kama vile ushairi hasa miongoni mwa vijana, maendeleo katika nyimbo za akina mama vijijini, mashairi simulizi yanayotongolewa radioni na kusikika mahali pengi katika Afrika mashariki na kuibuka kwa sanaa za maonesho simulizi na vichekesho katika televisheni na radio. Katika tanzu andishi, tutaangalia zaidi mashairi, tamthilia, hadithi fupi na riwaya zinavyojadili masuala mbalimbali kuhusu maisha ya Waswahili hasa miaka hii ya utandawazi.
Hali ya Fasihi Simulizi Fasihi simulizi ni aina ya fasihi ambayo kuwapo kwake hutegemea sana masimulizi ya mdomo. Fasihi hii ndiyo kongwe zaidi duniani, na ndiyo mzazi wa fasihi andishi. Jamii zote zenye maandishi zilikuwa, na bado nyingine zinaendeleza usimulizi. Kupitia katika fasihi hii, wanajamii husimuliana matukio, huelimishana, huonyana na kupeana taarifa za makuzi na malezi kwa njia ya kisanaa na ubunifu bila ya kutumia maandishi. “Njia ya kisanaa na ubunifu” ndiyo maneno ya msingi ambayo huyafanya masimulizi haya kuwa ya kifasihi. Kwa hiyo, si kila masimulizi ni fasihi, ila tu yale yatumiayo njia ya kisanaa na ubunifu mkubwa.
Katika miaka ya hivi karibuni utolewaji wa fasihi hii hasa nchini Tanzania umekumbwa na mabadiliko makubwa. Mabadiliko hayo ni matokeo ya kukua kwa teknolojia na matumizi ya vyombo vya kielektroniki. Kutoka katika hali ya kuonana wakiwa pamoja, msimuliaji na wasimuliwaji, sasa fasihi hii imeingia katika kuhifadhiwa kupitia katika televisheni au radio. Imeweza kuwekwa katika kanda na katika santuri na video ili wale ambao hawakuwapo wakati wa usimuliaji waendelee kuisikia au kuona masimulizi husika, muda mwingine.
Kwa mfano, kukua huku kwa teknolojia tunaweza kukuona kama hivi: ingawa nchini Tanzania televisheni imekuwapo tangu mwaka 1973 (Zanzibar), Tanzania bara, televisheni imeanza mwaka 1994 kama asemavyo Martin Sturmer katika utafiti wake (1998). Akifafanua hoja hiyo, Moore (1996) anaonesha kuwa kupingwa kwa televisheni Tanzania bara na kuwapo kwa Radio moja (RTD) tokea miaka ya baada ya uhuru kulikuwa ni mkakati wa serikali kujenga utamaduni wa Umoja, Udugu na Utanzania kupitia katika lugha ya Kiswahili. RTD ilijenga na kuuendeleza kwa makini utamaduni huu. Ndani yake, ilijenga fasihi ya Kiswahili na kuendeleza lugha sanifu ya Kiswahili. Katikati ya miaka ya 1980, malengo makuu ya kuujenga Utanzania yalikuwa yamefikiwa, ikiwa ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya watu wanaojua kusoma na kuandika barani Afrika. Kwa hiyo mwanzoni mwa miaka ya 1990 kama tulivyosema awali, viongozi wa Tanzania waliona wakati ulikuwa umetimia wa kuruhusu radio nyingi na vituo kadhaa vya televisheni.
Leo hii nchini Tanzania kuna televisheni 8, Radio 38, na magazeti 71 kati ya haya, yale ya kila siku yakiwa 18. Ni katika vyombo hivi vya mawasiliano ambapo fasihi simulizi hupitia ili kuwafikia wananchi. Katika televisheni kwa mfano, kipindi maarufu cha “mama na mwana” kilichokuwa kikirushwa na Radio Tanzania, sasa kimebadilishwa na msimuliaji (mama) anaonekana akiwa na watoto, studioni. Watoto wengine walioko nje ya studio wanaweza kumwuliza maswali na wakashirikiana na watoto wenzao kuimba nyimbo au kupiga makofi. Tunaweza kuuona mchango wa mwanamke katika makuzi ya watoto ukiendelezwa kwa njia za kisasa. Tunaweza kuona namna usimuliwaji wa fasihi simulizi ulivyojibadilisha kukubaliana na hali ya kisasa.
Mitaani, nyimbo simulizi katika muziki wa kizazi kipya au kama wauitavyo “bongo fleva” (Taz. www.bongoflava.com; na Sakawa, 2012) unaendeleza sio uhamasishaji tu, bali elimu na mawaoni na mjadala kuhusu siasa, kujilinda na magonjwa, kujadili changamoto za kila siku na mambo yanayowagusa hasa vijana. Katika TV, filamu za Kiswahili na michezo ya kuigiza, inapendwa sana na wananchi mitaani. Wananchi wa kawaida na wale wa kipato cha chini wameendelea kuipata fasihi hii kwa namna ya kipekee. Mapenzi yao kwa fasihi simulizi yamesababisha wachuuzi na wajasiriamali kufungua vituo vya kuonesha filamu hizo kwa malipo. Vituo hivi si vile vilivyo rasmi. Wale ambao hawana TV majumbani hukusanyika na kurundikana katika vyumba ambavyo vina TV na kuona filamu au vichekesho hivyo kwa malipo kidogo. Tunaweza kulinganisha “utamaduni” huu uliojengeka na ule wa wananchi wa nchi za magharibi wa kwenda kuangalia sinema katika majumba ya sinema.
Kama vilivyo vituo hivyo vinavyopendwa sana, mashairi na nyimbo radioni ni tanzu ambazo zimetawanyika katika jamii nyingi za Tanzania kupitia vituo vya FM ambavyo huwamo karibu katika kila mkoa. Kwa sasa kuna mikoa 30 na wilaya 146. Kwa hiyo kuwapo kwa radio 38 nchini Tanzania ni ishara kuwa kuna mabadiliko makubwa ya njia hii ya upashanaji habari. Kupitia katika radio hizi, fasihi simulizi, ingawa imebadilika kutoka katika gamba la zamani, bado inabeba dhima ile ile: kuwafanya watu wasikie sauti na kupata ujumbe wa kisanaa na uliojaa ubunifu mkubwa. Bado watu wengi wanaendelea kupata hadithi katika Kiswahili, na kuimbiwa mashairi kupitia katika radio hizi.
Yasemwayo na Fasihi Simulizi Kwa ujumla, kupitia katika vyombo hivi vikubwa yaani Radio na TV, mambo kadhaa huzungumzwa kuhusu yale yanayozigusa jamii. Kwa mfano, kupitia katika vyombo hivi, Tanzania nzima imeshiriki katika kuelewa mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi yaani, Albino yanayotokea hasa katika mikoa ya Shinyanga na Mwanza. Nyimbo zimetungwa kupinga ukatili huu. Nyimbo zimetungwa kuhamasisha watu kuelewa kinachoendelea na kupinga imani za kishirikina. Mashairi katika mashule yamesikika yakiitetea sauti ya Albino ili apate haki ya kuishi na haki ya elimu katika mazingira ya amani.
Jambo jingine ambalo sasa linajadiliwa kifasihi ni lile la kuhimiza watu kuvumiliana pamoja na kuwa na imani za dini tofauti. Kuwapo kwa dini tofauti hakukuwahi kuwa ni suala la kujadiliana nchini Tanzania. Hata hivyo, hivi karibuni vitendo vya kupigana, kuuana na chuki vimeanza kujitokeza kuzungukia masuala ya kidini. Kwa hiyo, mara moja jamii imeanza kujieleza kupitia katika fasihi simulizi. Yapo mashairi kadhaa sasa ambayo yanapaza sauti kupinga uhusiano huu mpya miongoni mwa wanajamii ambao kimsingi ni ndugu. Katika mikutano mbalimbali, ikitokea kuna vikundi vya waimbaji, basi hutakosa kusikia nyimbo kuhusu kuvumiliana na kupendana kwa watu wa dini tofauti. Nyimbo hizi zinasikika si katika vituo vya FM tu, bali pia katika TV zinazokuwa zimejitokeza kurekodi matukio. Dhamira hii ya kutokugombana kwa sababu za kidini ni mpya katika fasihi ya Kiswahili.
Mbali ya dhamira hizi, dhamira ambayo sasa imejisimika na kuwa na mizizi katika jamii ni ile inayojadili ugonjwa wa UKIMWI. Nyimbo, mashairi, ngonjera na michezo ya kuigiza imeanza kulizungumzia janga hili hasa kutokea mwishoni mwa miaka ya 1980 (Taz. Mutembei, 2001 na 2002). Kwa sasa nyimbo mbalimbali kuhusu UKIMWI, dalili zake, madhara yake na hasa jinsi ya kuepukana nao zinaimbwa karibu kila mkoa. Kwa hiyo, miaka ya sasa inaona kuwa fasihi simulizi imejitanua kutoka katika dhamira za zamani kama vile kupinga ufukara na ujinga, na kujielekeza katika mambo ya zama hizi kama ilivyoelezwa. Hata hivyo, hii haimaanishi kuwa yale mambo ya zamani yameachwa. La hasha! Ufukara bado ni mjadala miongoni mwa vijana hasa katika nyimbo zao za kizazi kipya. Basi mbali na dhamira hizi, kuna suala la kisiasa hasa kuhusu vyama na utawala.
Katika siasa, nyimbo za kizazi kipya zinaongelea sana suala hili. Labda kuingia bungeni na kuwa mbunge wa kuchaguliwa, mwimbaji wa nyimbo hizi amezipa hadhi nyimbo za bongo flava. Leo hii, vijana wanaimba na kujadili kuhusu maana na kushiriki kwa vyama vingi katika siasa za Tanzania. Wanaimba kuhusu mabadiliko ya Katiba na upatikanaji wa Katiba Mpya Tanzania. Suala ambalo pia sasa linajadiliwa ni maana na muundo wa Muungano wa Tanzania. Dhamira hii haikupata kuwapo kabla. Ilikuwa haiyumkiniki wananchi kuongelea muungano. Wakati fulani ilichukuliwa kama kosa kubwa na mwiko. Sasa nguvu ya fasihi simulizi imevunja mwiko huu na serikali imeruhusu mjadala kuwapo. Haya ni machache kuhusu dhima ya fasihi simulizi katika zama hizi nchini Tanzania. Dhamira hizi pia zinaonekana katika fasihi ya maandishi.
Yasemwayo na Fasihi andishi Kwanza, watu wengi wamekuwa na mwamko wa kuandika kuliko ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hii pia inatokana na kuwapo kwa uwezekano wa kuchapishwa kazi za waandishi. Zamani uchapishaji ulikuwa ni wa mashaka. Maendeleo katika teknolojia, hasa matumizi ya Kompyuta kwa upande mmoja; na kushamiri kwa biashara kama matokeo ya soko huria, kumesababisha wafanyabiashara kujiingiza katika eneo hili la utoaji, uuzaji na usambazaji wa maandishi. Leo hii kuna wachapishaji wengi wa vitabu na magazeti.
Katika magazeti (ambayo kama ilivyooneshwa, kuna zaidi ya magazeti 71) kuna hadithi fupi na mashairi. Baadhi ya hadithi fupi huwa na mfululizo wa matoleo ambapo kwa kila toleo la gazeti kuna mwendelezo wa hadithji ile ile. Kutoka katika mfululizo wa aina hii, waandishi maarufu kama Eric Shigongo (Taz. www.globalpublishers.info) wamejitokeza ili kuhamasisha watu kubadilika kutoka katika ufukara. (Taz. www.youtube.com/watch?v=1nV4AGsqOgo). Kutokana na kushiriki kwa watu kama hawa, vijana wananunua magazeti na kusoma, wakitaka kujifunza namna ya kuishi maisha ya kitajiri.
Mbali na hadithi fupi, kona za mashairi zimeendelea kupewa nafasi katika magazeti. Hadithi fupi hujadili mambo ya muda mrefu, na visa na mikasa ambayo imekuwapo katika jamii kwa kipindi kirefu. Haya hivyo, mashairi hujadili matukio ya hivi karibuni. Ni kama ambavyo tunaweza kuangalia habari kuhusu matukio motomoto ambayo yanatokea wakati huo (breaking news), ndivyo inavyotokea katika mashairi. Hii haina maana kuwa mashairi yameacha kujadili dhamira zilizoota mizizi katika jamii. La hasha! Dhamira hizo bado hujadiliwa na mashairi. Lakini matuko na habari moto moto huelezwa kifasihi na mashairi zaidi kuliko hadithi fupi au riwaya.
Mbali na mashairi na hadithi fupi, riwaya (au hadithi ndefu) zimekuwa na mambo kadhaa kifasihi. Kutoka yale ya kubuni na kuwa ya kifalsafa (kama ya Kusadikika na Mzimu wa Watu wa Kale) leo hii kuna yale yanayogusa mambo ya vijana kama riwaya ya Dunia Yao (Said Ahmed Mohamed Khamis, 2006) ambapo mwandishi anajadili masuala mengi kuhusu vijana katika ulimwengu wa Waswahili wa zama hizi.
Licha ya dhamira kuhusu UKIMWI, (riwaya za Kisiki Kikavu, Ua la Faraja, Hadithi za Kiafrika: kwa wahubiri na walimu, ni mifano michache), katika riwaya, sasa kuna dhamira mpya. Katika Makuadi wa Soko Huria (2002) Chachage anaandika kuhusu madhara ya kujiingiza katika soko huria bila kujiandaa na kuwa na watu wachache waliojaa ufisadi ambao unaiangamiza jamii iliyoinukia katika maelewano ya kijamaa. Kuna mjadala biashara ya madini (mfano, riwaya ya Pesa za Mawe, ya Oscar Ulomi, 2006). Hili ni suala ambao limeendelea kuitikisa jamii ya Kitanzania hadi sasa. Licha ya madini, kuvumbuliwa kwa gesi na mafuta kumetokeza sauti ya washairi katika mashairi hasa yanayotokeza sasa magazetini.
Aidha, dhamira nyingine ni kuhusu biashara haramu ya madawa ya kulevya na madhara yake kwa jamii (Taz. Watoto wa mama Ntilie, 2002 cha E. Mbogo). Mchambuzi anaweza kuona mabadiliko katika jamii ya Tanzania kwa vitabu hivi vitatu: Kile cha Chachage kinachoongelea ufisadi, cha Ulomi cha biashara ya madini na cha Mbogo kuhusu madawa ya kulevya. Hali hii ni tofauti na Fasihi ya Tanzania iliyokumbatia Ujamaa na kusisitiza umoja na maelewano miongoni mwa jamii. Kwa hakika, uandishi wa Karumuna Mboneko (2004) katika Pambazuko Gizani, unaonesha mabadiliko kama hayo miongoni mwa asasi za kidini. Mabadiliko makubwa yanatokea sasa ambapo baadhi ya watu wamefanya Kanisa kuwa aina ya biashara. Hivyo kuna mfumuko wa makanisa mengi ya “uamsho”. Kutokana na shida za kijamii na za kibinafsi, wanajamii wengi wana hitaji la kisaikolojia na kimaadili. Watu wamekata tamaa ya maisha mazuri, na kuporomoka kwa maadili kumezidisha huzuni miongoni mwa watu. Kwa hiyo, wimbi la makanisa yanayoombea watu kupata neema na maisha mazuri limekuwa kubwa. Hata hivyo, kama asemavyo Karumuna, viongozi wa Makanisa haya wengi wamewakatisha tamaa waumini wao, pale ambao ama wamejihusisha katika maisha kinyume cha maadili yao, au wameshikwa na kushitakiwa kuhusu biashara haramu waliyoiendesha “nyuma ya altare”. Mambo haya ni dhamira mpya kabisa katika fasihi andishi.
Licha ya dhamira hizi, suala la ushirikina bado limeendelea kuwa katika dhamira moto moto za fasihi andishi. Kwa mfano, Gabriel Ruhumbika anaandika kuhusu ushirikina katika riwaya ya Janga Sugu la Wazalendo, 2002. Na katika hadithi yake iliyochapishwa mtandaoni na wachapishaji wa Lulu, Lutatinisibwa Kamala anaadika kuhusu Mauaji ya Albino (2010). Ni mauaji ambayo msingi wake ni imani za kishirikina kuhusu kupata utajiri wa haraka.
Dhamira hii ya utajiri wa haraka kwa njia za kishirikina inakuzwa zaidi na kuwapo kwa filamu hasa kutoka Nijeria (Nollywood) ambazo zinatafsiriwa kwa Kiswahili na kurushwa katika TV. Kama nilivyosema awali, watu wengi hasa vijijini huziangalia filamu hizi ambazo baada ya kutafsiriwa huwekwa katika kanda za video na kuuzwa. Waendesha biashara ya video pembezoni mwa miji na vijiji vyenye umeme, huwavutia sana hasa vijana kwa kuonesha filamu hizi kwa malipo kidogo.
Kuchapishwa kwa tamthilia ya Changamoto (E. Mahenge, 2010) kunaingiza dhamira nyingine mpya inayoshughulikia haki za watu wenye ulemavu katika jamii. Suala hili lina uhusiano mkubwa na imani za kishirikina na mauaji ya albino kwa upande mmoja na mfumuko wa uingizwaji na utazamwaji wa filamu za Kinijeria kama ilivyoelezwa. Masuala haya yana uhusiano na maisha ya jamii za Watanzania kutaka utajiri usio wa kufanya kazi, ambao ni kasumba iliyomo katika maisha ya biashara huria. Uliberali na uliberali mambo leo unaoenezwa kupitia katika utandawazi umebadilisha maisha ya wanajamii wengi kutaka kuwa matajiri bila ya kuhangaikia utajiri huo.
Hitimisho Fasihi ya Tanzania, kama yalivyo maisha ya wakati huu inaakisi matokeo ya utandawazi. Iwe ni fasihi simulizi au fasihi andishi, namna zote zinayaangalia maisha ya Watanzania kama yaliyo njia panda. Kutoka katika maisha yaliyosisitiza watu kukaa pamoja na kupendana wakati wa Ujamaa, sasa kuna maisha ya ubinafsi. Kutoka katika maisha ya watu wengi kuwa na ufukara wa vitu, sasa kuna maisha yanayodanganya kuhusu uwezekano mkubwa wa watu kuwa na utajiri wa mali kwa muda mfupi. Mambo haya, si tu yaandikwa katika kazi za kifasihi na kusimuliwa katika mashairi na hadithi, bali pia yanaoneshwa katika filamu ndani ya televisheni. Ni maisha ambayo yanadhihakiwa kupitia katika vichekesho ndani ya radio na katika televisheni. Kutokea kwa vikundi vingi vya vichekesho ni njia ya wasanii ya kupunguza hali ya ukataji tamaa iliyozikumba jamii maskini za Kitanzania. Ni njia pia ya kuwacheka wale wanaokimbilia utajiri huku hawataki kufanya kazi.
Fasihi ya Kiswahili katika Tanzania, na labda katika Afrika ya Mashariki inapita katika kipindi cha mabadiliko. Suala hili pia linaakisi mabadiliko katika ujamii na katika elimu na siasa. Kumekuwapo na hamu ya watu wengi zaidi kutaka kusoma. Hali hii imesababisha kuwapo kwa shule nyingi za sekondari na vyuo vingi, hata pale ambapo hakuna walimu au vifaa na miundo mbinu ya kutosha. Kila mtu anataka elimu. Hili si suala baya, lakini linahitaji maandalizi.
Fasihi inajadili mwamko huu mpya katika elimu na kaangalia maandalizi duni. Inajadili madhara ya kutokuwa na elimu na kukimbilia katika imani za kishirikina. Imani ambazo zinaondoa haki za wale wenye ulemavu na kuingiza woga katika familia. Woga huu, ndio unaochukuliwa na viongozi wa makanisa mapya ili kuwatia moyo waumini wao, kuwarudishia hali ya kupenda kuishi, huku viongozi hao wakijitajirisha kwa pesa za sadaka na mavuno mengine. Haya yote yanaongelewa katika fasihi ya Kiswahili ambayo imejipatia dhamira mpya kwa jinsi jamii inavyopita katika kipindi cha mabadiliko.
Baadhi ya Marejeleo
- 1. Moore, D. (1996). Reaching the villages: Radio in Tanzania. Journal of the North American Shortwave Association.
- 2. Sturmer, M. (1998). The Media History of Tanzania. Ndanda Mission Press).
- 3. Finnegan, R. (1970). Oral Literature in Africa, Oxford: Clarendon Press
- 4. Okpewho, I. (1992). African Oral Literature. Backgrounds, Character and Continuity, Bloomington: Indiana University Press
- 5. Sakawa, D.K. (2012). Entertainment-Education Communication Strategy in Tanzania: The Efficacy and Efficiency of Bongo Flava TV programs in Youth behavior influence, LAP Lambert Academic Publishing, Saarbrucken, Germany
No comments:
Post a Comment