Maofisa wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (PTA) wakishuhudia wakati mabasi ya Kampuni ya usafiri wa mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (UDART) yalipokuwa yakishushwa kutoka katika meli jijini Dar es Salaam leo hii asubuhi. Jumla ya mabasi 70 yalipokelewa.
Sehemu ya kupita mabasi hayo ikiandaliwa wakati wa ushushaji wake kutoka katika meli ya Kichina.
Moja ya mabasi hayo likitoka katika meli.
Moja kati ya mabasi hayo likiwa limetoka katika meli.
Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, Charles Newe, akizungumza na waandishi wa habari wakati wa kupokea mabasi hayo.
Na Dotto Mwaibale
KAMPUNI ya usafiri wa mabasi ya mwendo kasi jijini Dar es Salaam (UDART), imeingiza nchini mabasi mapya 70 kutoka China kwa ajili ya kuongeza nguvu ya usafirishaji abiria.
Akizungumza wakati wa upokeaji wa mabasi hayo Bandarini jijini Dar es Salaam leo Mkurugenzi Mtendaji wa UDART, Charles Newe alisema hiyo ni hatua nzuri kwa kampuni hiyo yenye lengo la uhakika wa kutoa huduma bora ya usafiri kwa abiria jijini.
Alisema mabasi hayo yataongeza ufanisi wa usafirishaji wa abiria hivyo kuwapunguzia adha ya usafiri wakati wa jiji la Dar es Salaam.
Alisema mabasi hayo yataongeza uchumi wa nchi na kutoa ajira kwa wananchi na kupunguza gharama ya usafiri ambapo kwa wale wenye magari wataacha kuyatumia magari yao kwenda kazini ambapo wataokoa sh.8000 katika kila sh.10000 waliyokuwa wakiitumia kwa siku kununulia mafuta.
"Wenye magari sasa hivi watakuwa wanaokoa sh.8000 kila siku ambapo watakuwa wakitumia mabasi yetu kwa sh.2000 tu kuja kazini na kurudi majumbani kwao" alisema Newe.
Alisema kiasi hicho cha fedha kitakachookolewa kitaweza kwenda kufanya shughuli zingine za maendeleo ya nchi na mtu mmoja mmoja.
Akizungumzia mabasi hayo alisema yanauwezo wa kubeba watu kuanzia 150 hadi 160 na kuwa bei ya basi moja ni limenunuliwa kwa dola za Marekani 260,000 na kuwa mabasi hayo yanafikisha idadi ya mabasi 210 huku mahitaji ya mabasi hayo ikiwa ni 305 kwa awamu ya kwanza.
Alisema changamoto kubwa iliyokuwepo ni uchache wa mabasi yaliyokuwepo ambapo watu walilazimika kupanda kwa wingi lakini kwa ongezeko la mabasi hayo itasaidia kupunguza changamoto hiyo.
No comments:
Post a Comment