VURUGU kubwa zilizowalazimisha Polisi kutumia helikopta kuzituliza,
zilitokea jana baada ya baadhi ya wakazi wa Kata ya Kibiti kuvamia kituo kidogo
cha jeshi hilo wakitaka kukichoma moto katika kile kilichoelezwa kuwa ni kutaka
kulipiza kisasi cha mwenzao kukamatwa na polisi na kisha kupigwa hadi kufariki
dunia juzi.
Katika
vurugu hizo, wakazi hao wengi wao wakiwa ni vijana, walifunga Barabara ya Kilwa
kwa zaidi ya saa tatu hivyo kukwamisha usafiri wa kwenda na kutoka mikoa ya
Mtwara na Lindi.
Vurugu hizo hazikuishia hapo kwani
vijana hao walivamia nyumba za askari wa kituo hicho na kisha kutoa vyombo na
kuviharibu. Katika tukio hilo, nyumba moja ilichomwa moto.
Hali ilivyokuwa
Kamanda wa Operesheni Maalumu ya Jeshi
la Polisi nchini, Saimon Sirro alisema katika tukio hilo, nyumba hiyo ya jeshi
imeteketezwa kabisa kwa moto na vyumba vinne vya nyumba nyingine walizopanga
askari wengine jirani vimevunjwa... “Vijana hao walikuwa wakiingia na kutoa
vyombo na nguo za askari waliopanga humo na kuzichoma moto.”
Kamanda
Sirro alisema vurugu hizo zilitokea baada ya kupatikana kwa taarifa za kifo cha
Hamis Athumani (30), mkazi wa Kibiti katika Hospitali ya Taifa Muhimbili
alikokuwa amepelekwa kutibiwa majeraha ambayo kamanda huyo alisema marehemu
alidai kuyapata baada ya kupigwa na askari waliomkamata alipojaribu kuwatoroka
walipomkamata kwa tuhuma za kuhusika na dawa za kulevya.
Alisema
kukamatwa kwake kulitokana na operesheni ya msako wa bangi na dawa za kulevya.
Akizungumzia tukio hilo, shuhuda mmoja wa
tukio hilo ambaye hakutaka jina lake liandikwe alisema baada ya kipigo hicho,
kijana huyo alilalamika maumivu na hivyo ndugu zake walifika kituoni hapo na
kumpeleka Kituo cha Afya Mchukwi.
“Hali
yake iliendelea kuwa mbaya na akapelekwa Muhimbili ambako alifariki dunia jana
alfajiri,” alisema shuhuda huyo na kuengeza: “Taarifa hizo zilipofika kijijini,
baadhi ya vijana walikusanyika na kuanza kuhamasishana na kuanza kuziba
barabara kwa matairi na kuvamia nyumba za askari na kuchoma moto.”
Baada
ya ghasia hizo kupamba moto, jeshi liliamua kutumia helikopta ambayo ilitua
Kibiti saa 5.50 asubuhi ikiwa na askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU),
wakiongozwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Mathei.
Kamanda Sirro alisema watu 18
wamekamatwa kwa kuhusika na vurugu hizo.
Chanzo
cha vurugu
Inadaiwa kuwa Jumanne saa tatu usiku,
askari wa Kituo cha Polisi Kibiti walivamia kambi ya vijana wanaodaiwa
kujishughulisha na biashara ya dawa za kulevya inayojulikana kwa jina la Kosovo
iliyopo Mbebetini karibu kabisa na Sekondari ya Kibiti.
Askari
hao ambao baadhi ya wakazi wa Kibiti wamewaeleza kuwa ni mashujaa kwa hatua yao
ya kuthubutu kuvamia kambi hiyo ambayo inadaiwa kushindikana kwa muda mrefu
kushughulikiwa na askari wa Kituo cha Polisi Kibiti, walikumbana na upinzani
mkali wa vijana wapatao 30 wakipinga kukamatwa kwa kiongozi wao.
Inadaiwa
kuwa baada ya kumkamata, walimshambulia kwa virungu lakini kutokana na upinzani
mkali waliopata kutoka katika kundi hilo, walishindwa kuondoka naye lakini
walimwacha akiwa mahututi.
Habari
hizo zilieleza kuwa vijana hao walimchukua kiongozi wao na kumpeleka Mchukwi
kwa matibabu kabla ya kumsafirisha kwenda Muhimbili ambako alifariki dunia.
Baada
ya kupatikana kwa taarifa za msiba huo, baadhi ya wananchi wa Kibiti
waliandamana saa 1.22 asubuhi hadi kituo cha Polisi ambako waliharibu pikipiki
tatu za polisi. Walitawanywa baadaye kwa baruti na silaha za moto.
Baadaye, polisi kutoka Ikwiriri walifika
na kudhibiti kundi kubwa la watu hao wapatao 120 kwa mabomu ya machozi.
Askari
afariki
Askari wa Kikosi cha Kutuliza ghasia
(FFU) H21 PC Domick, amefariki dunia na wenzake wanne kujeruhiwa vibaya, baada
ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Kibaha Pwani kuelekea Rufiji kutuliza
vurugu hizo kupinduka katika eneo la Mkuranga.
|
No comments:
Post a Comment