MAELFU ya wanywaji wa pombe hasa pombe kali, wako katika hatari
kupata magonjwa ya ini na upofu wa macho kutokana na kufurika kwa pombe
‘feki’ katika maeneo mbalimbali nchini ambazo huzinywa.
Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi Jumapili katika
mikoa mbalimbali nchini, umebaini kuwa watu hao hununua pombe hizo feki,
zinazotengenezwa kienyeji vichochoroni na kuwekwa katika chupa na
‘viroba’ zilizo na nembo za kampuni halisi zi nazozalisha pombe hizo.
Pombe hizo feki huuzwa katika hoteli, baa,
grosari, vibanda vya pombe za kienyeji na meza za wafanyabiashara
ndogondogo zilizogaa maeneo yenye mikusanyiko ya watu ikiwamo masoko na
vituo vya mabasi.
Uchunguzi huo umebaini kuwepo kwa mtandao wa
vigogo, wanaojihusisha kuhujumu viwanda na kampuni zinazotegeneza pombe
hizo nchini kwa kutengeneza pombe feki.
Pombe zinazotengenezwa kienyeji na mtandao huo wa
wafanyabiashara wakubwa na baadhi ya watu waliokaribu na vigogo wa siasa
nchini ni pamoja aina ya Whisky, Vodka, Valuer, Gin, Konyagi na Kiroba
Original.
Uchunguzi umebaini kuwa kazi hiyo ya kutengeneza
pombe feki inafanyika katika mikoa ya Mwanza, Dar es Salaam, Arusha,
Kilimanjaro na Singida.
Jijini Dar es Salaam kazi hiyo inafanyika katika maeneo ya Manzese, Tandika na Kitunda.
Mmoja wa wakazi wa Dar es Salaam, John Kwilasa
mkazi wa Mbezi Beach Mtaa wa Yekeyeke alisema kuwa baadhi ya wanawake
huuza konyagi feki hasa za paketi maarufu kama viroba.
“Siku hizi kuna konyagi feki zinauzwa pale mtaani
kwetu. Kuna siku nimeagiza nikaletewa kiroba, nilipokunywa nikashangaa
kusikia ladha nyingine. Nilipowauliza wenzangu nikaambiwa huwa kuna
pombe feki, niwe makini,” alisema Kwilasa.
Mfanyabiashara Chriss Martin anayefanya biashara
katika miji ya Mwanza, Moshi na Dar es Salaam, alisema kuwa kuzagaa kwa
pombe hizo ni matokeo ya rushwa katika vyombo vya usimamizi wa bidhaa.
“Juzi juzi nilikuwa Dar es Salaam, nikaagiza pombe
aina ya gordon’s na nilipoiweka tu mdomoni nikagundua ni feki, maana
hata ladha siyo yenyewe. Niliimwaga na hili ni tatizo, liko miji mingi
tu nchini,”alisema.
Uchunguzi unaonyesha kuwa pombe kali
zinazotengenezwa kienyeji na kujazwa kwenye chupa za vinywaji halisi ni
zile ambazo hupendwa na wanywaji nyingi kati ya hizo zikiuzwa kwa bei
nafuu.


No comments:
Post a Comment