TAARIFA YA KAIMU MKUU WA MKOA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAADHIMISHO YA
WIKI YA MAJI KITAIFA TAREHE 16-22/2013 MKOANI LINDI.
Ndugu
Waandishi wa Habari na Wananchi wote wa Mkoa wa Lindi;
Napenda kuwafahamisha kuwa Mkoa wetu umepewa
heshima na Wizara ya Maji kuwa Mwenyeji wa maadhimisho ya 25 ya Wiki ya Maji Kitaifa
yatakayo anza tarehe 16 Machi, 2013 na kufika kilele tarehe 22 Machi, 2013.
Shukrani
Napenda kuishukuru Wizara
ya Maji kwa kutupa heshima ya kuwa wenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya 25 ya
Wiki ya Maji.
Aidha, navishukuru sana
Vyombo vya Habari kwa kufika katika mkutano huu na kuwa tayari kutangaza
mafanikio yaliyowekwa katika Sekta ya Maji.
Naamini maadhimisho haya
yatakuwa chachu kwa wadau mbalimbali kuchangia kwa hali na mali katika ujenzi, uendeshaji
na matengenezo ya miradi ya maji Mkoani wa Lindi.
Utangulizi;
Kila mwaka kuanzia mwaka 1988, Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki
ya Maji kuanzia tarehe 16-22 Machi kwa kuwahusisha wananchi na wadau wote
wa maji.
Kilele cha maadhimisho huwa ni tarehe 22 Machi ambayo siku hiyo
inafahamika Kimataifa kuwa ni Siku ya Maji Duniani kwa mujibu wa Azimio Na.
193/47 la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Uzinduzi utafanyika tarehe 16 Machi 2013 katika Kijiji cha Mtandi Wilaya
ya Kilwa na Kilele cha Maadhimisho kitakuwa tarehe 22 Machi 2013 katika
Manispaa ya Lindi kwenye Uwanja wa Ilulu. Mgeni Rasmi katika Kilele cha
Maadhimisho atakuwa ni Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. JAKAYA
MRISHO KIKWETE.
Maadhimisho ya Wiki ya Maji ya mwaka huu yataongozwa na Kauli Mbiu
isemayo “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI KITAIFA”.
Madhumuni ya Maadhimisho;
Madhumuni ya Maadhimisho ya wiki ya maji ni pamoja na:-
Kuwaelimisha wananchi kuhusu Sera ya Maji na majukumu yao katika
kuitekeleza.
Kutathmini maendeleo ya Utekelezaji wa Programu ya Maji, hali ya
huduma ya maji na usafi wa mazingira na kuweka mikakati ya kuboresha utoaji wa
huduma na uhifadhi wa rasilimali za Maji.
Kuhamasisha wananchi na wadau wengine kushiriki katika
kupanga, ujenzi, uendeshaji na matengenezo ya miradi ya maji na usafi wa
mazingira.
Kujenga mshikamano miongoni mwa wadau mbalimbali wa Sekta ya Maji.
Kutoa ujumbe kwa wadau kuhusu Kauli Mbiu ya Wiki ya Maji na Siku
ya Maji Duniani.
Madhumuni hayo yanalenga kuboresha utoaji wa huduma ya
Maji, Usafi na Uhifadhi wa Mazingira, pamoja na usimamizi na utunzaji wa
rasilimali za Maji nchini (vyanzo vya maji na miundombinu ya kufikisha huduma
ya maji kwa watumiaji).
Maandalizi ya maadhimisho ya Wiki ya Maji
mwaka 2013;
Maandalizi ya Maadhimisho ya Wiki ya Maji yanaendelea vizuri na uzinduzi
na kilele cha maadhimisho kitawahusisha viongozi wa Kitaifa.
Maadhimisho ya mwaka 2013 yanakusudia kuwashirikisha wananchi katika:-
kupanga, kujenga, kuendesha na kufanyia matengenezo miradi ya maji na kuimarisha
usafi wa mazingira,
kutunza vyanzo vya maji na kuwaelimisha wananchi juu ya matumizi
endelevu ya rasilimali za maji.
Matukio haya yataenda sambamba na kutoa ujumbe (maudhui) wa Siku
ya Maji Duniani ya mwaka 2013 ambao ni “MWAKA WA USHIRIKIANO WA MAJI
KITAIFA”.
Shughuli zitakazofanyika katika Wiki ya Maji hapa Mkoani Lindi ni pamoja
na:-
Kuzindua miradi 3ya Maji
vijijini ambayo ujenzi wake umekamilika.
Vijiji hivyo ni Mtandi (Wilaya ya Kilwa), Rondo Mnara (Halmashauri ya
Wilaya ya Lindi) na Luchelegwa (Wilaya ya Ruangwa).
Miradi hii imetekelezwa kupitia Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji
na wadau mbalimbali.
Kuzindua Mradi wa
Uboreshaji Huduma ya Maji katika Mji wa Lindi kutoka chanzo kilichopo katika
eneo la Kijiji cha Sinde.
Kutakuwa na Mikutano ya
Hadhara maeneo yote ya Uzinduzi
Miradi yote itakayozinduliwaitawanufaisha
wananchi wapatao 134,108.
Kugharamia Maadhimisho;
Ili kuweza kugharamia maadhimisho ya Wiki ya Maji mwaka 2013, Wadau
mbalimbali wameombwa kutoa michango ya hali na mali ili kufanikisha maadhimisho
haya.
Maadhimisho ya kitaifa ya Wiki ya Maji yanagharimiwa na Wizara ya
Maji , Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Mamlaka za Maji Safi na Maji taka nchini, Halmashauri,
Taasisi na Mashirika mbalimbali ya Kiserikali na yasiyo ya Kiserikali na
Watumiaji Maji.
Napenda kuchukua fursa hii kuwaomba wadau wote kutoa michango ya hali na
mali ili kuweza kufanikisha maadhimisho haya ya Wiki ya Maji Kitaifa
yatakayofanyika hapa Mkoani kwetu mwaka huu wa 2013.
Wito kwa Wananchi wa Lindi;
Nitoe wito kwa wananchi wa Mkoa wa Lindi kuwapokea na kuwakaribusha wageni
wote ambao watakafika Mkoani kwetu kwa nyakati mbalimbali katika Maadhimisho ya
Wiki ya Maji Duniani. Kipekee ninawaomba Wananchi/Wakazi wa Manispaa ya Lindi
kujitokeza kwa wingi kumlaki Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania
atakapowasili tarehe 21 Machi, 2013 na kuendelea kuwa nae mpaka siku ya Kilele
cha Maadhimisho katika Uwanja wa Ilulu tarehe 22 Machi, 2013.
No comments:
Post a Comment