RAIS mteule wa Kenya, Uhuru Kenyatta
amewashukuru wananchi pamoja na Mwenyezi Mungu kwa kumwezesha kushinda nafasi
hiyo huku akiahidi kuijenga upya Kenya.
Uhuru amesema ataweka kipaumbele kwenye
kutunza rasilimali za nchi na kuhakikisha zinawanufaisha wananchi wote, pia
kuwawezesha wanawake na vijana.
Katika hotuba yake aliyotoa muda mfupi
baada ya kutangazwa mshindi jana, Kenyatta alisema anawashukuru wagombea
alioshirikiana nao katika mchakato wote wa uchaguzi na kuwakaribisha kuungana.
“Nawashukuru wagombea wenzangu wote kwa
kujitolea kwa moyo kushiriki katika kinyang’anyiro hiki kwa kuwa jambo hilo
limezidi kuonyesha demokrasia iliyopo nchini,” alisema.
Aliongeza kuwa anaahidi kushirikiana
vyema na wagombea hao akiwamo Raila Odinga kwa ajili ya kuijenga upya nchi yao,
akiwakaribisha na kuwataka waondoe kinyongo kutokana na ushindi alioupata.
“Tulianza zoezi zima kama timu na
nitashirikiana nanyi kama timu, ikiwamo kuhakikisha tunafuata yale yote
yaliyopo kwenye katiba hususan kuhakikisha kila mwananchi anapata haki yake
anayostahili.”
Kiongozi huyo pia aliwashukuru watu
mbalimbali waliofanikisha uchaguzi huo kwenda vyema ikiwamo vyombo vya habari
katika nchi hiyo ambavyo vilikwenda sambamba katika kuripoti matukio yote ya
uchaguzi, pamoja na vyombo vya usalama vilivyosimamia chaguzi hizo.
“Usalama bado ni tatizo katika nchi
yetu, lakini ningependa kuvishukuru vyombo husika kwa kufanikisha tunavyozidi kuendelea
suala hilo litakuwa vizuri,” alisema. Uhuru alieleza hayo baada ya Tume Huru ya
Mipaka na Uchaguzi (IEBC) kumtangaza kuwa mshindi katika uchaguzi uliofanyika
Machi 4 akiwa amegombea kwa tiketi ya muungano wa Jubilee.
Uhuru aliibuka mshindi katika uchaguzi
huo kwa kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizohitajika ili kupata ushindi
kulingana na mahitaji ya Katiba Mpya ya nchi. Matokeo yaliyotolewa na IEBC
yanaonyesha kuwa Uhuru alipata kura 6,173,433 ambazo ni asilimia 50.07 huku
mpinzani wake Raila Odinga akipata 5,340,546 ambazo ni asilimia 43.28.
Kwa ushindi huo, Uhuru amepata idadi
kubwa ya kura inayohitajika na Katiba Mpya ambayo ni zaidi ya asilimia 50+1 na
kuzuia uwezekano wa kurudiwa kwa uchaguzi. Uhuru pamoja na mgombea mwenza wake,
William Ruto wamepata ushindi huo huku wakiwa wanakabiliwa na mashtaka katika
Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kuhusiana na ghasia za baada ya uchaguzi
mkuu wa mwaka 2007.
Ushindi
huo umepingwa na mpinzani mkuu wa Uhuru, mgombea urais kupitia muungano wa Cord,
Raila Odinga ambaye amesema ‘kamwe
hawatayatambua’ na kuahidi kuyapinga mahakamani. Akizungumza muda mfupi baada ya kutangazwa
kwa matokeo hayo, Odinga alisema anajiandaa kwenda mahakamani kupinga matokeo
ya urais yaliyompa ushindi Uhuru. Odinga, aliwaambia waandishi wa habari kuwa
matokeo yaliyotolewa na tume hiyo yalikuwa yamehujumiwa hasa baada ya kutokea
hitilafu katika mitambo ya elektroniki iliyokuwa inatumiwa katika shughuli
hiyo.
“IEBC imerudia makosa yaleyale ya uchaguzi
mkuu wa 2007, kwa kuwa tuna mahakama tunayoiamini tunaomba watu wetu watulie
hadi mahakama itakapotoa uamuzi. Wenzetu pia wajiepushe na aina yoyote ya
ghasia,” alisema. Alisema kwamba hana tatizo la kushindwa iwapo ameshindwa
kihalali, lakini kwa matokeo haya ana jukumu kubwa la kupinga mahakamani ili
kulinda mahitaji na heshima ya wapiga kura.
Aidha, alisema kugoma kwa mitambo
hiyo kulichanganya mambo katika shughuli ya kuhesabu kura. Alisema kuwa baada
ya kutokea hitilafu, kura alizokuwa amepata katika maeneo bunge ambayo ni ngome
zake, ziliongezwa kwenye hesabu ya kura za muungano pinzani wa Jubilee. Siku
moja kabla ya kutangaza matokeo hayo, IEBC ilikiri kuwa matatizo
yaliyosababishwa na mtambo wake wa kupeperusha matangazo ni pamoja na kuongeza
mara nane kura zilizoharibika.
Baadhi ya wananchi walieleza kuwa
na wasiwasi kuhusu idadi kubwa ya kura zilizoonekana kuharibika, kwani zilikuwa
kura zaidi ya 300,000 ambapo kwa sasa zimepungua mpaka kufika idadi ya kura
80,000, baada ya kuhakiki kura hizo kwa mara ya pili.
Pingamizi lao lilikataliwa Mapema wiki hii, wakati shughuli ya kuhesabu
kura za urais ilikuwa inafanyika, wanaharakati walifungua kesi mahakamani
kutaka uchaguzi usimamishwe kutokana na hitilafu mbalimbali zilizotokea ,
lakini mahakama kuu ilitupilia mbali kesi yao ikisema kuwa haina uwezo wa
kufanya uamuzi katika kesi hiyo, na kuwa ni mahakama ya juu zaidi pekee
inayoweza kusikiliza kesi hiyo.
Matokeo hayo na mivutano yote iliyopo kwa sasa vinatokea baada ya siku
tano tangu Wakenya kupiga kura kuchagua rais, magavana, maseneta, wabunge,
wawakilishi wanawake na wawakilishi wodi. Tume ya uchaguzi ilichukua zaidi ya
saa tano kukagua hesabu ya kura hizo kabla ya kutangaza matokeo hayo jana
mchana.
Kwa mujibu wa maagizo yaliyopo katika Katiba Mpya ya nchi hiyo, mshindi
wa uchaguzi anatakiwa kutangazwa iwapo tu ametimiza masharti ya kikatiba ya
kutangazwa kuwa rais wa nne wa Kenya. Pamoja na ushindi wa kura kwa zaidi ya
asilimia 50 lazima awe ameshinda asilimia 25 katika nusu ya kaunti zote 47
nchini Kenya.

No comments:
Post a Comment