Pamoja na kuwa Rais na prodyuza mkuu wa mfuko wa Unity Productions,
Michael Wolfe (aliyezaliwa 3 Aprili 1945, Marekani) ni mtunzi wa vitabu
vya kishairi, hadithi za kubuni, za masafa na historia. Pia ni mhadhiri
wa masuala ya kiislamu katika vyuo vikuu nchini Marekani, vikiwemo kile
cha Harvard, Georgetown, Stanford, SUNY Buffalo, na cha Princeton. Ana
shahada ya fani ya fasihi (sanaa) kutoka Chuo Kikuu cha Wesleyan.
Ana asili ya dini mbili, Uyahudi kutoka kwa baba na Ukristo kutoka
mama yake. Hivyo alikuwa na fursa ya kusherehekea sikukuu zote Hanukkah
na Krismasi. Anaandika:
“Baba yangu ni Myahudi, mama ni ni Mkristo. kutokana na
uchotara wangu, mguu mmoja upo katika Uyahudi na mwengine upo katika
Ukristo. Imani zote zilikuwa hazina mashaka kwangu. Hata hivyo, ile
iliyokuwa inahamasisha ‘wao wao tu’ (waliobarikiwa) [Uyahudi] niliiona
haiungani mkono nami, na ile nyengine iliyojaa mafumbo [Ukristo]
haikunifurahisha”
Kutembea kwake kwingi na kupenda vitabu kulimfanya kuufahamu Uislamu
ambao kani (nguvu ya uvutano) yake ilishindwa kuzuiliwa na Michael.
Moja ya sababu iliyomfanya akubaliane na Uislamu ni kukuta katika
Uislamu mambo yanayoendana na matakwa yake. Hivyo anasema:
“Sikuweza kuorodhesha mahitajio yangu yote, lakini
angalau nilikuwa najua kipi nikifatacho. Dini niitakayo mimi ni dini
itakayoweza nieleza kuhusu metafizikia (falsafa ya kuchunguza chanzo cha
uhai na maarifa) kwani metafizikia ndiyo sayansi. Sitaki ile
inayopongeza utumizi duni wa akili, au iliyojaa mafumbo ili kuwaridhisha
wachungaji. Isiyokuwa na wachungaji (viongozi), isiyokuwa na tofauti
kati ya uasili na vitu vyake vilivyobarikiwa. Ambapo kutakuwa hakuna
vita na nyama. Tendo la ndoa liwe ni la asili tu na sio eti kutokana na
laana waliyopewa viumbe. Mwishowe, nilitaka ibada ya kila siku
itakayoongoza nidhamu yangu. Zaidi ya yote, nilitaka jambo lililo wazi
na uhuru wa kweli. Sikutaka niwe katika mkumbo wa kufata vitu kibubusa.*
Na kila nilivyokua nausoma Uislamu, ndivyo ulivyokuwa ukiafikiana na
matakwa yangu.”
Michael wolfe amekuwa Muislamu akiwa na miaka 40, baada ya kushindana
na imani tofauti tofauti kwa miaka 20. Ingawa inatosha kwa mtu kufanya
Hijja mara moja tu katika maisha, Bw. Wolfe katika kugombania kwake
kupata radhi za Mwenyezi Mungu, amehiji si chini ya mara tatu, Hijja
yake ya mwanzo ikiwa mwaka 1991. Akiuona ukweli wa Uislamu na ujinga wa
baadhi ya watu katika faida ya Uislamu, Michael aliona haja ya kuandika
haya:
“Rafiki zangu walioathiriwa na siasa hawakuridhishwa na
chaguo langu jipya. Wote walichanganya Uislamu na viongozi madhalimu wa
Mashariki ya Kati waliodhaniwa kutaka kufanya mapinduzi ili watawale.
Vitabu walivyosoma, habari walizotazama vyote vilichukulia dini hii kama
mpango wa kisiasa tu. Halikuwapo linalosemwa kuhusu ibada zake. Napenda
kumkariri Mae West kwao pale alivyosema: “Muda wowote utakaochukulia dini mzaha, basi wewe ndio utakayechekwa.”
Kihistoria, Muislamu anaiona dini kama ni hitimisho, mmea uliopevuka
ambalo ulipandwa tangu wakati wa Adam. Imejengwa kwa msingi wa kuabudu
Mungu mmoja kama Uyahudi, ambayo mitume wake Uislamu unawachukulia kama
ni ndugu waliotoka kumoja na kilele chao kikiwa Yesu na Muhammad. kusema
kweli, Uislamu umefanya kazi kubwa katika hatua ya kuirudisha ladha ya
maisha kwa mamilioni ya watu. Kitabu chake, Qur’an kilimfanya Goethe
kusema, “Mnaiona hii, mafundisho yake hayashindwi abadan; pamoja na
mifumo yetu yote ya kibinaadam, hatuwezi kufika, na huo ndio ukweli
hakuna mfumo wa kibinaadamu utakaofanikiwa”.
 |
Mashaallah! |
Akiongea na mtangazaji Bob Faw kuhusu imani yake mpya. Faw ‘alimpiga’
bwana Wolfe kwa swali hili: “Kwa kuwa ushakuwa muislamu, je kuna
tofauti yoyote kwako labda!?” Wolfe akajibu: “Bila shaka ipo, umbile
nilokuwa nalikosa zamani maishani mwangu lipo sasa nami. nalihisi
kabisa.” Wolfe alivutiwa sana na mafundisho ya Uislamu kuwa kila mtu
azungumze na Mungu mwenyewe, bila kuwa na kizuizi katikati:
“Hili jambo la kufanya mazungumzo na Mola wako mtukufu
bila kuwa na balozi katikati, kusikohitaji jengo fulani au mtu maalum,
kunanipendeza mno.”
 |
Michael Wolfe |
Michael Wolfe anajulikana zaidi kwa filamu yake katika kipindi cha
Nightline cha ABC iliyorushwa Aprili 18, 1997 ikijulikana kama
An American in Mecca (
Mmarekani Akiwa Makkah).
Kipindi hiko kikateuliwa kuwemo katika tuzo za Peabody, Emmy, George
Polk na National Press Club. Filamu ilishinda tuzo ya mwaka kutoka
katika Baraza la Waislamu (Muslim Public Affairs Council). Michael Wolfe
alishiriki kutengeneza, na kusimamia uhariri wa filamu ya masaa mawili
iliyohusu maisha ya Mtume Muhammad iliyoitwa
Muhammad: Legacy of a Prophet.
Filamu hiyo ilioneshwa nchi nzima na PBS na baadae kuonyeshwa kimataifa
na National Geograpghic International. Filamu ilituzwa na Cine Special
Jury Award kwa filamu bora izungumziayo watu au mahali. Wakati
wakutengeneza filamu hiyo, washiriki walihitaji kuperuzi kwingi katika
maisha ya Mtume.
Michael Wolfe mwenyewe anakiri kusoma Ibn Kathir na vitabu vyengine vya seerah (mwenendo wa Mtume).
Kiukweli, kukawa na Wamarekani wengi ambao walisilimu baada ya kuona
filamu hii. Katika mahojiano, Islam Online walimuuliza alichovuna baada
ya zoezi hili kubwa la kuandaa filamu hii ya Muhammad na alijibu kama
ifuatavyo:
“Nimemjua Mtume vyema zaidi kuliko mwanzo kabla
hatujaanza kutengeneza filamu hii japokuwa kumsoma kwangu ndio kwanza
kulianza. Kuna mengi ya kujifunza. Wakati tunatengeza filamu hii,
niliweza kuona na kufahamu hali ya Waislamu wa Marekani. Najua sasa wepi
ni Waislamu na vipi tunafanya. Ni kifungua jicho kwangu mimi kama
Mmarekani niliyezaliwa hapa, ni jambo la faraja sana kukutana na watu
kutoka sehemu mbalimbali, watu wenye lugha tofauti na mengineyo. Ni moja
ya hazina za kuwa Muislamu.”
Katika mahojiano tofauti, Michael Wolfe kama mmoja wa waandaaji wa filamu ya
Muhammad: The Legacy of a Prophet, alisema:
“Kwa Wamarekani wengi kutokuwa na uelewa wa imani yangu kunanishangaza sana.
Japokuwa Uislamu ni dini inayokua kwa kasi zaidi, bado tabia nyingi za
Wamarekani kuhusu Uislamu zimekuwa zikitawaliwa na chuki, kuelewa vibaya
na hata wakati mwengine uhasama wa wazi. Wana uelewa mdogo tu kuhusu
Mtume aliyefundisha dini hii na ipi ni misingi ya ibada zetu. Siasa na
mila za watu wa mashariki ya Kati, gumzo la ugaidi vyote vimeshiriki
kukandamiza uelewa wao mzuri wa dini. Ukichukulia kwamba kundi kubwa la
Waislamu haliko hata Mashariki ya Kati bali Indonesia, utambuzi huu sema
kweli uanapotosha.”
Filamu nyengine alizoshiriki Wolfe katika uandaaji ni
Cities of Light: The Rise and Fall of Islamic Spain (
Miji ya Muangaza: Kupanda na Kuporomoka Kwa Dola ya Kiislamu Hispania) na
Prince Among Slaves (
Mfalme Miongoni Mwa Watumwa).
Sanjari na hilo, Wolfe ameshiriki katika vipindi mbalimbali vya redio.
Anaandika makala maalumu iitwayo “From A Western Minaret” kwa ajili ya
jarida la mtandaoni Beliefnet.com.
 |
Michael Wolfe kwenye vazi maalum la hijja. |
Kazi zilizochapishwa za Wolfe ni pamoja na
The Hadj: An American’s Pilgrimage to Mecca. (New York: Atlantic Monthly Press, 1993. Kina kurasa 352);
One Thousand Roads to Mecca: Ten Centuries of Travelers Writing about the Muslim Pilgrimage, (New York: Grove Press, 1997. Kina kurasa 656) ; na
Taking Back Islam: American Muslims Reclaim their Faith,
(Rodale Press, Pennsylvania, 2003. Kina kurasa 256). Baadhi ya tuzo
alizopokea ni pamoja na Lowell Thomas Award, “Best Cultural Tourism
Article, 1998”; Marin County Arts Council Writers Award, 1990, na 1983;
California State Arts Council Writers Award, 1985. Michael Wolfe
alitangazwa mshindi wa Tuzo ya 2003 ya Wilbur Award kwa kitabu bora cha
mwaka kuhusu dini. Anaishi mwishoni mwa mtaa salama, uliofungwa, huko
Santa Cruz.
[* Kamusi ya TUKI imetafsiri neno ‘dogma’ (ububusa) kama imani
inayofundishwa katika kanisa unayotakiwa kuikubali bila kuisaili
(kuhoji).].
No comments:
Post a Comment