NA ALI MOHAMED ZANZIBAR
Magendo ni vitendo viovu vinavyohusisha uingizaji au usafirishaji wa bidhaa au mazao kwa njia zisizo halali/kisheria kwa lengo la kukwepa kodi na kukiuka sheria ambapo ni njia haramu ya kufanya biashara. Sababu kuu za magendo ni tamaa ya utajiri, ujinga na kukosa uzalendo.
Ni dhahiri kuwa magendo yana athari kubwa kwa maendeleo ya nchi na Wananchi wake, huikosesha serikali mapato ambayo ndio yanayohitajika katika kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu, afya, maji safi na salama, ujenzi wa miundombinu ya barabara na huduma nyengine muhimu.
Karafuu ni zao kuu la uchumi wa Zanzibar linalosaidia upatikanaji wa fedha za kigeni na kuiwezesha Serikali kuimarisha huduma za jamii. Katika kipindi cha miaka ya 1980 na 2010 zao hili lilikuwa katika changamoto kubwa ya kusafirishwa kwa magendo. Baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu walikuwa wakisafirisha zao hili kwa magendo kwenda katika nchi za jirani.
Katika wakati huo usafirishaji magendo wa zao la karafuu ulikuwa mkubwa kiasi cha kuzifanya nchi hizo za jirani kuwa wauzaji wakubwa wa zao la karafuu kwa zaidi ya tani 2,000 katika soko la dunia huku ikizingatiwa kuwa katika nchi hizo hakuna mikarafuu inayolimwa.
Wakati nchi hizo zikionekana kuuza karafuu kwa kiwango hicho, uzalishaji wa zao hilo kwa Zanzibar ulishuka kutoka tani 9,952 hadi tani 2673 katika kipindi cha miaka kumi, sababu moja ikiwa ni karafuu za Zanzibar kusafirishwa kwa magendo kwenda katika nchi hizo za jirani.
Katika kipindi hicho cha mwaka 2000 hadi 2010, Zanzibar ilipoteza kiasi cha dola za kimarekani milioni 16, sawa na TZS bilioni 34.7 kutokana na usafirishaji karafuu kwa magendo.
Kwa mujibu wa sheria ya ZSTC ya mwaka 2011 kifungu cha 9 (a) Wakulima na Wafanyabiashara wa zao hilo la karafuu wanatakiwa kuuza karafuu zao Serikalini tu kupitia Shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) ambayo ni taasisi pekee iliyopewa mamlaka ya kununua na kuuza karafuu, hivyo kufanya magendo ya karafuu ni makosa.
Kulikuwa na sababu nyingi zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya watu ikiwemo suala la bei ya karafuu kuwa ndogo na kusababisha watu kuamua kuziuza karafuu zao kimagendo nje ya nchi kwa lengo la kutafuta bei nzuri.
Kwa lengo la kuimarisha, kulinda ubora na kuwahamasisha Wakulima kuuza karafuu zao Serikalini kupitia vituo vya ununuzi vya ZSTC badala ya kusafirisha kwa magendo, mikakati mbali mbali ilipangwa na kutekelezwa na Serikali.
Mwaka 2011 Serikali ilitoa ahadi na kuitekeleza ahadi hiyo ya kuwalipa Wakulima wa zao la karafuu asilimia 80 (80%) ya bei ya karafuu ya soko la dunia. Karafuu za daraja la kwanza zinanunuliwa kwa bei ya TZS 14,000 kwa kilo badala ya TZS 5,000 kwa kilo, bei iliyokuwepo mwaka 2010. Ongezeko hili ni sawa na asilimia 180.
Kadhalika, vituo vipya vya ununuzi na uuzaji wa karafuu vimejengwa, vituo vya zamani vimekarabatiwa ambapo idadi kamili ya vituo vyote ni 35 Unguja 3 na Pemba 32, huduma zote muhimu zimeimarishwa kwenye vituo hivyo na ulinzi pia umeimarishwa zaidi katika kudhibiti magendo.
Mkakati mwengnie uliochukuliwa ni kwa Shirika la ZSTC kujipanga vyema katika suala la upatikanaji wa kifedha kwa wakati na kulipa fedha taslim kwa Wakulima wa zao la karafuu na kuhakikisha hakuna Mkulima anaekopwa karafuu zake anapokwendwa kuuza.
Utekelezaji wa mikakati hiyo imesaidia sana kufanikiwa kudhibiti magendo ya karafuu, hivi sasa Wananchi wanauza karafuu zao katika vituo vya ununuzi vya ZSTC. Ni jambo la kuwashukuru na kuwapongeza Wakulima, Wananchi na Vikosi vya Ulinzi na Usalama kwa kazi nzuri walioifanya ya kushirikiana na Serikali katika kupambana na magendo ya karafuu.
Pamoja na mikakati na jitihada hizo zilizochukuliwa na Serikali kudhibiti magendo ya karafuu kufanikiwa kwa kiwango kikubwa lakini inaonekana kuwa bado wapo watu wachache wanaendeleza biashara hiyo haramu. Katika msimu wa mavuno mwaka 2015/2016 gunia 33 za karafuu kavu na gunia 31 za makonyo zimekamatwa ambazo zilikuwa zinasafirishwa nje.
Lakini kabla Mkulima hajafikiria suala la kuuza karafuu zake kwa njia ya magendo, anapaswa kwanza ajiuulize masuali yafuatayo;-
Ni nini anachotaka zaidi ilhali karafuu zimeongezwa bei na bei hiyo ni kubwa zaidi ya huko anakokwenda kuuza kwa magendo?
Pia kwa nini anafanya magendo llhali pamoja na bei nzuri lakini pia faida ya karafuu ikirudishwa ndani ya nchi ndio hupatikana elimu bora kwa mwanawe, afya bora kwake, barabara nzuri kwa wote, maji safi kwa kila mtu na maendeleo kadhaa wa kadhaa?
Inakuwaje mtu anajitia katika magendo ya karafuu ilhali uwezekano wa kupoteza maisha yake ni mkubwa au uwezekano wa kukamatwa na kufungwa na kupoteza utumishi wake kwa familia yake na kuitia katika mateso, kwa nini anafanya hivyo?
Ni kwa sababu gani za msingi watu ambao wanauwezo wa kupata kiasi kikubwa cha fedha kwa kuuza karafuu zao serikalini waingie katika tombola ya kukosa kabisa kwa kujaribu kuingia kwenye magendo na kuhatarisha mali zao kwa kuzama baharini au kufilisiwa na kubaki katika umaskini kwa kukosa fedha za Serikali na zile ambazo walizitarajia kuzipata kwa kuuza magendo huko nchi za jirani?
Ni wazi kuwa anachokosa mtu huyo ni uzalendo na uwezo mzuri wa kufikiri.
No comments:
Post a Comment