Mkurugenzi
Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, John Wanga, akizungumza wakati wa kukabidhi
madawati katika Manispaa hiyo.
Halmashauri
ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza, imekabidhi madawati 2,600 kwa shule zote
74 za Msingi za umma zilizopo kwenye manispaa hiyo, ikiwa ni sehemu ya
utekelezaji wa agizo la Rais Dkt.John Pombe Magufuli la kutaka kila wilaya
kumaliza tatizo la madawati ifikapo Juni 30 mwaka huu.
Madawati
hayo ambayo yametengenezwa kwenye karakana ya shule ya sekondari ya wavulana ya
Bwiru, ni sehemu ya mpango wa kutengeneza madawati 9,080 na hivyo kumaliza
kabisa tatizo la uhaba wa madawati katika manispaa hiyo.
Akikabidhi
madawati hayo hii leo, Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, John Wanga,
amesema madawati hayo yametengenezwa kutokana na fedha zitokanazo na makusanyo
ya ndani pamoja na michango ya wadau wengine ambapo katika mgawo wa awali, kata
zote 19 za manispaa hiyo zimepewa madawati 139 kila moja.
Wanga
amesema kila dawati moja lenye uwezo wa kukaliwa na wanafunzi watatu,
limegharimu shilingi 98,000 ambapo manispaa ilinunua vifaa ikiwemo mbao,
misumari na vyuma na kulipa gharama za ufundi zinazofikia shilingi 15,000 kwa
kila dawati na kwamba madawati mengine yaliyobakia kukidhi mahitaji yanaendelea
kutengenezwa kwenye karakana hiyo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Manju Msambya, amepiga marufuku matumizi
ya madawati hayo kwenye shughuli nyingine ikiwemo mikutano ya kisiasa huku
akiwataka wazazi,walezi na jamii nzima kwa ujumla kutambua umuhimu wa kuchangia
juhudi za kuboresha elimu.
Renatus
Mulunga ambae ni Mstahiki Meya wa Manispaa ya Ilemela amesema halmashauri hiyo
inafanya kila jitihada kuhakikisha kwamba inatatua tatizo la upungufu wa
madawati kwa shule za msingi katika manispaa hiyo, hatua ambayo itasaidia
kuboresha ari ya wanafunzi kujisomea.
Utengenezaji wa Madawati ya Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza,
ukiendelea katika karakana ya Shule ya Sekondari ya wavulana Bwiru.
No comments:
Post a Comment