Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa
Katiba kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutekelezwa kwa Sheria
ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 inayolenga kuimarisha
utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini. Kulia kwake ni
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa wizara hiyo Sheiba Bullu.
Na.
Fatma Salum – Dar es salaam.
Serikali
imeanza kutekeleza Sheria ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya
mwaka 2016 (The Whistleblower and Witness Protection Act. 2016) ili kuimarisha
utawala bora na mapambano dhidi ya uhalifu nchini.
Hayo
yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi Utekelezaji wa Katiba kutoka Wizara ya
Katiba na Sheria, Bw. Kamana Stanley wakati akizungumza na waandishi wa habari
leo jijini Dar es Salaam kuhusu kuanza kutumika kwa sheria hiyo.
Stanley
amesema kuwa kuwepo kwa sheria hiyo
kutasaidia kuwapatia ulinzi wa kisheria wale wote wanaotoa taarifa za uhalifu
wa makosa ya aina mbalimbali wanayoshuhudia yakitendeka. Vilevile itarahisisha
utoaji na upatikanaji wa taarifa za uhalifu kwani sasa taarifa hizo zitatolewa
na kupokelewa sio tu kwenye vyombo vya dola pekee bali pia kupitia vyombo vya
habari na vyanzo vingine vinavyobainishwa katika sheria hiyo.
“Wananchi
wasiwe na woga kujitokeza kutoa taarifa za uhalifu na matendo ya aina zote
yanayofanywa kinyume cha sheria kwani taarifa hizo zitakuwa siri na zitafanyiwa
kazi bila ya kuwataja watoa taarifa. Pia mashahidi wanapotakiwa kufika
mahakamani wasiogope kwani sheria hii inawalinda” amesema Stanley.
Amefafanua
kuwa wahusika watakaoshindwa kushughulikia vyema taarifa zinazotolewa kwao na
kuruhusu watoa taarifa na mashahidi kupata madhara, sheria hiyo imeweka
utaratibu wa namna ya kushughulika nao.
Aidha,
Stanley ameeleza kuwa katika sheria hiyo wale ambao taarifa zao zitafanikisha kuokoa
mali ya umma, kupatikana kwa wahalifu na kulinda mazingira na maisha ya
binadamu kutokana na uhalifu uliopangwa kufanyika, wamewekewa utaratibu wa
kupatiwa motisha ikiwa ni pamoja na kuwafidia wale ambao wataathirika kutokana
na taarifa walizotoa.
Stanley
ameongeza kuwa Serikali inatarajia kwamba kutungwa kwa sheria hii kutaleta
matokeo chanya katika kupambana na uhalifu wa aina zote hivyo kukuza ari ya
wananchi kusimamia wenyewe juhudi za kujiletea maendeleo.
“Masuala
ya usimamizi wa utawala wa sheria yataimarika kutokana na kuwepo kwa utayari wa
wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya uhalifu kwa kufika katika vyombo
vya sheria kutoa ushahidi. Pia ushiriki wao katika kufichua maovu yakiwemo
yanayosababisha hasara kwa taifa utasaidia kuinua uchumi ukizingatia kwamba
sasahivi Serikali inapambana sana na mafisadi” ameeleza Stanley.
Sheria
ya Kuwalinda Watoa Taarifa za Uhalifu na Mashahidi ya mwaka 2016 (The
Whistleblower and Witness Protection Act. 2016)imeanza rasmi kutumika Julai Mosi
mwaka huu baada ya kuidhinishwa na Waziri mwenye dhamana ya usimamizi wa sheria
Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe.
No comments:
Post a Comment