Na Ahmed Abdullaziz Lindi.
MTU Mmoja amefikishwa mahakama ya wilaya ya Lindi akikabiliwa na Shitaka moja la kumjeruhi kwa kumchoma na moto wa pasi mke wake.
Mwanzaga Degratius Mbowi (44), amefikishwa mahakamani hapo na kusomewa
Shitaka lake na mwanasheria wa Serikali, Mwahija Ahamadi.
Akimsomea Shitaka lake mbele ya Hakimu mkazi mfawidhi
wa mahakama hiyo, Dustan Ndunguru, mwendesha mashiataka huyo akadai kuwa mei 27
mwaka huu, saa 1:30 asubuhi,huko mtaa wa Wailes katika Manispaa ya
Lindi,mshitakiwa alimjeruhi kwa kumchoma moto mke wake wa ndoa Olifoncia
Chembe.
Mwahija aliiambia mahakama hiyo kwamba siku na wakati
huo mshitakiwa na mke wake huyo wote kwa pamoja walikuwepo nyumbani kwao na
mara kukatokea kidogo mifarakano ambayo yalimpelekea mshitakiwa kumpiga na
hatimaye kuchukua pasi ya moto na kumuunguza mlalamikaji mkono wake wa kulia na
sehemu nyingine.
Pia mwendesha mashitaka huyo alidai kwamba kutokana na
kitendo hicho,mshitakiwa amemsababishia mlalamikaji maumivu makali kwenye
mwili wake.
Aidha, Mwahija aliiambia mahakama hiyo kwamba kutokana
na kitendo hicho mshitakiwa amefanya kosa chini ya kifungu cha 225 kanuni ya
adhabu sura ya 16.
Mshitakiwa amekana kosa linalomkabili na amepelekwa
rumande,baada ya upande wa mashitaka kupinga dhamana kwa mshitakiwa kutokana na
kutopata taarifa ya maendeleo ya mlalamikaji, kesi hiyo namba 49/2012, itatajwa
tena Juni 11 mwaka huu.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment