WAZIRI wa Uchukuzi Dk.Harrison Mwakyembe amewasimamisha kazi Wakurugenzi wanne wa Shirika la ndege la ATCL kutokana na kukiuka sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma ambao umetishia uhai wa shirika hilo muhimu hapa nchini.
Hayo yamebainika leo hii jijini Dar es Salaam, kwenye taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na kusainiwa na katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng. Omar Chambo.
Waliosimamishwa kazi ni Kaimu Mkurugenzi wa Uhandisi, John Ringo, Mwanasheria wa ATCL Amini Mziray, Kaimu Mkurugenzi wa fedha, Justus Bashara na Kaimu Mkurugenzi wa Biashara Josephat Kagirwa.
Aidha taarifa hiyo ilibainisha kuwa ili kazi ziweze kuendelea Mheshimiwa Waziri amemteua Kapteni Lusajo Lazaro, kukaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, kuanzia tar 5 juni mwaka huu.
Awali Mh.Waziri alimteua Paul Chizi kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, hata hivyo utaratibu wa uteuzi wake haukufuata sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma. Hivyo kupitia sheria namba 8 ya mwaka 2002 na kanuni za utumishi wa uma za mwaka 2003Na.17(4), Mheshimiwa Waziri ametengua uteuzi huo kutokana na sheria hiyo kumpa mamlaka ya kufanya hivyo.
mwisho.
No comments:
Post a Comment