WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda ametaka Katiba Mpya impunguzie Rais
madaraka hasa katika nafasi ya uteuzi.
Kauli hiyo ya Pinda inapingana na ile iliyotolewa
na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue kuhusu Katiba Mpya ambaye
aliiambia Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba madaraka ya Rais yasiguswe
akisema kama atanyang’anywa, atashindwa kuongoza nchi. Balozi Sefue
alisema nafasi ya Rais inapaswa kuwa imara na yenye uwezo wa
kuwaunganisha Watanzania wote.
“Asilimia kubwa ya Watanzania, wamekuwa
wakipendekeza Rais apunguziwe madaraka aliyonayo, jambo ambalo linaweza
kuleta hatari mbeleni, suala hili linatupasa kuwa nalo makini,” alisema
Balozi Sefue na kuongeza:
“Tusiwe wepesi wa kutamka maneno bila ya
kutafakari hasara na faida zake, tunapaswa kutambua taifa letu lenye
miaka 51 ya Uhuru bado maskini, kuna mataifa yenye miaka 200 hadi 400,
lakini kamwe hayathubutu kumpunguzia Rais madaraka.”
Hata hivyo, jana Pinda aliiambia tume hiyo ya
Mabadiliko ya Katiba: “Kuna haja ya kumpunguzia Rais madaraka kwani
amekuwa na mzigo mkubwa wa kuongoza Serikali. Kitu kikubwa ambacho
ningependa kiangaliwe kwenye Katiba Mpya kwa upande wa madaraka ya Rais
ni katika uteuzi wa viongozi mbalimbali.”
“Nimetaka Katiba Mpya impunguzie mzigo Rais kwani
amekuwa na kazi nyingi sasa ni vyema angepunguziwa mzigo huo hasa katika
masuala ya uteuzi wa viongozi.” Pinda alitoa mfano kwamba katika
kazi ya uteuzi wa viongozi, Makamu wa Rais anaweza kumsaidia kazi hiyo
kwa kushirikiana na vyombo vingine ambavyo Katiba itaviainisha.
Mbali na hayo, Pinda alitaka pia Katiba Mpya izuie
wabunge kuwa mawaziri na Serikali za Mitaa ziwekewe mfumo sahihi wa
kujiendesha na kuwe na tume itakayoshughulikia masuala ya Muungano,
lakini akataka Muungano ubaki wa Serikali mbili.Mwananchi. |
No comments:
Post a Comment