KAMPUNI ya Mad Mad Entertainment iliyopo
jijini London nchini Uingereza, imeanzisha program maalum ya kupeleka wasanii
wa filamu za bongo nje ya nchi kwa lengo la kukuza sanaa hiyo hapa nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar
es Salaam leo, Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo Yasmin Razak alisema ameamua
kufanya kazi na wasanii hao ili kuleta
mabadiliko na kuwakwamua kiuchumi wasanii wa filamu hapa nchini.
“Kwa muda mrefu niliokaa London sioni kama
sanaa hii ina maendeleo, nikafikiria kitu gani nifanye ili kukuza tasnia hii, katika mkataba na kampuni
msanii atakayetengeneza filamu na wasanii wa nje atalipwa kiasi cha sh 50
milioni pamoja na malipo mengine yatakayokuwepo kwenye mkataba, ikiwa ni pamoja
na asilimia fulani kwa kila kazi itakayouzwa hapa nchini.
“Nimekuwa nikifanya kazi hiyo na wasanii
wengi kutoka Nigeria wakiwemo kina Omotola, Two Face na wengineo na pia Ghana,
Congo na hata Uingereza, hivyo nimeonelea kuwa itakuwa vema Tanzania nao
kuingia katika mchakato huo,”alisema Razak.
Razak ambaye amewahi kufanya kazi ya
filamu na Fally Ipupa, alitaja vigezo
vya msanii atakayechaguliwa ikiwa ni pamoja na umaarufu, kuijua lugha ya kiingereza, uwezo wa kuigiza
na kuuvaa uhusika wowote pamoja na mavazi.
Naye rais wa Shirikisho la Filamu
Tanzania, Simon Mwakifamba aliwataka wasanii hao kujipanga katika kuhakikisha
wanaingia kwenye ushindani huo na kuwataka wale watakaochaguliwa kujituma na
kuonyesha nidhamu ya uhakika.
“Hapa kuna kuinua vipaji, soko la
kimataifa na mengineyo, hivyo ni vema kufanya kazi kikamilifu kwa wale
watakaochaguliwa na si kujisahau, wanatakiwa wasanii watatu na tupo katika
hatua za awali za mchujo,” alisema Mwakifwamba.
Naye muigizaji Issa Musa maarufu kama
Cloud, alisema kuwa lugha itakuwa ni tatizo kubwa kwa wasanii walio wengi, hivyo
kuitaka kampuni hiyo iangalienamna ya kuweza kuwasaidia wasanii hao.
No comments:
Post a Comment