| Waandishi wa habari za michezo waliojitokeza kwenye mkutano huo leo wakifuatilia kwa makini maelezo ya Malinzi. |
| Waandishi wa habari za michezo wakifuatilia mkutano huo. |
| Malinzi akisoma taarifa yake kwa waandisho wa habari za michezo. |
JAMAL
MALINZI
S.L.P 10000
DAR ES SALAAM
13/FEBRUARY/2013
TAARIFA
KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH:
KUENGULIWA KWANGU KUGOMBEA URAIS WA TFF 2013
Ndugu zangu,kupitia vyombo vyenu vya habari
ninaomba niueleze umma wa watanzania,hususani wadau wa mpira wa miguu,yafuatayo
kuhusu kuenguliwa kwangu.
Awali ya yote nieleze kusikitishwa kwangu
na maamuzi yaliyotolewa na kamati ya rufaa ya TFF ya kuniengua kugombea urais
wa TFF.Sikubaliani na maamuzi haya .
Katika kuniengua kamati ya rufaa ya
uchaguzi ya TFF imetoa sababu mbili (nanukuu magazeti ya jana tarehe 12/02/2013
maana hadi leo sijakabidhiwa barua ya kuenguliwa).
1.
Kukosa uadilifu kwa kupinga
waraka uliotolewa na TFF wa kubadili
Katiba ya TFF mwezi Desemba 2012.
2.
Kukosa uzoefu wa miaka mitano
ya uongozi.
Ndugu zangu,kiini cha maamuzi ya Kamati ya
rufaa dhidi yangu ni pingamizi lililowekwa na mtu mmoja anayeitwa AGAPE FUE.Bwana
Agape Fue aliniwekea pingamizi katika kamati ya uchaguzi akidai mimi nilipinga waraka wa kubadili
katiba ya TFF na pia sina uzoefu wa miaka mitano ya uongozi wa mpira.Kinyume na
matakwa ya kamati ya uchaguzi kama yalivyotangazwa kuwa mtoa pingamizi aje
mwenyewe kutetea pingamizi lake ,Bwana Agape Fue hakutokea mbele ya Kamati ya
Bwana Lyatto.Matokeo yake tarehe
31/01/2012 kamati ya uchaguzi ya
TFF ilitoa maamuzi ya ya kutupilia mbali pingamizi hili.
Bwana
Agape Fue hakuishia hapo kwa mara
nyingine tarehe 06/02/2013 alikata rufaa kwenye kamati ya rufaa ya uchaguzi
akidai kamati ya uchaguzi haikumtendea haki. Rufaa hii haikuwa na anwani wala
namba ya simu ya Bw.Agape Fue.Rufaa
ilisikilizwa tarehe 10/02/2013 na maamuzi ya kukata jina langu yakatangazwa
jioni ya tarehe 11/02/2013.
Mpaka leo najiuliza hivi huyu Bw. Agape Fue
ni mwanaume au ni mwanamke?(hakueleza
kama ni Bwana au Bibi Agape Fue). Agape Fue ni nani hasa? Anaishi wapi?Je ni
Mtanzania au sio Mtanzania maana kikanuni
wasio watanzania hawaruhusiwi kujihusisha na uchaguzi wa TFF (rejea
kifungu cha 9 cha kanuni za uchaguzi),pingamizi lake halikuambatana na
udhibitisha wa uraia. Kwa nini alichukua maamuzi haya? Sipati jibu. Iweje mtu achukue maamuzi mazito ya kumkatia mtu
rufaa kisha uishie kusaini karatasi na kuwaachia wengine wakusemee na usije
hata kushuhudia kinachoendelea kama kweli una maslahi na madai yako? Waandishi
wa habari mnisaidie kupata majibu.
Ndugu zangu ,mtoa pingamizi alidai haikuwa
sahihi kupinga azimio la kubadili katiba ya TFF kwa njia ya waraka.Naomba nisistize
mambo matatu:
1.
Wajumbe wa mkutano mkuu wa TFF
wanawakilisha matakwa ya vyama vilivyowatuma kwenda kwenye
mkutano mkuu wa TFF,na ndio maana
chama cha mpira cha mkoa wa Kagera (KRFA) kiliitisha kikao cha kamati ya
utendaji ili kamati iweze kutoa
mwongozo kwa wajumbe wake kuhusu nini
kifanyike kuhusu waraka ulioletwa na TFF,hivyo maamuzi yaliyotolewa ya kuukataa
waraka huu yalikuwa ni maamuzi ya chama cha mpira mkoa wa Kagera na wala
hayakuwa ni maamuzi ya Jamal Malinzi,iweje malinzi niadhibiwe kwa maamuzi
haya,kwa nini usiadhibiwe mkoa mzima na mikoa yote iliyopinga waraka?hii ni
haki kweli? Siamini kama kuna mjumbe wa mkutano mkuu aliyekiuka maamuzi ya
kamati yake ya utendaji.
2.
Katika mchakato wa kubadili
katiba kwa njia ya waraka kilichokuwa kinagomba sio maudhui (content) ya
mabadiliko ya Katiba bali utaratibu uliotumika kubadili Katiba. Swali la msingi
tulilojiuliza wajumbe wa kamati ya utendaji KRFA ni kwamba je kwa mujibu wa Katiba ya TFF
kifungu 22 na kifungu 30 wapi katiba inatamka kuwa inaweza kubadilishwa kwa
njia ya waraka? Mpaka leo hilo jibu hakuna,labda aliyeniwekea pingamizi
atusaidie kupata jibu la swali hili. Katiba ya TFF iko wazi kabisa
inatamka kuwa Katiba itabadilishwa kwa
njia ya Mkutano Mkuu tu (General Assembly).
3.
Ni kweli FIFA iliagiza
yafanyike mabadiliko ya Katiba ya kuingiza kipendele cha ‘club licencing’
katika Katiba ,lakini je FIFA katika agizo hilo ilisema Katiba ya TFF ivunjwe
ili kutimiza azma hiyo? Ikumbukwe kuwa mwaka 2004 FIFA iliagiza TFF iingize
kwenye Katiba kipengele cha Katibu Mkuu awe wa kuajiriwa badala ya
kuchaguliwa,agizo hili lilitekelezwa kwa kupitishwa na Mktano Mkuu wa TFF,iweje
leo utaratibu huu ukiukwe? Hata majuzi CAF walipotaka kubadili katiba ili Rais
wa CAF atokane na wajumbe wa Kamati ya Utendaji jambo hili lilitekelezwa kwa
kuitisha mkutano mkuu wa dharura uliofanyika Seychelles majuzi. Katiba ndio
msingi mkuu wa uendeshajiwa TFF,nitaipigania siku zote.Huo ndio utaratibu,si
CAF si FIFA si Vyama vya mpira vya nchi,hakuna anayebadili Katiba kwa njia ya waraka,kama kuna mwenye
ushahidi aulete.
Kuengua jina langu eti kwa
kuwa nilipinga waraka wa kubadili Katiba sio uamuzi sahihi.
Kuhusu uzoefu wa miaka
mitano katika Uongozi:
Ikumbukwe kuwa katika
uchaguzi mkuu wa TFF mwaka 2008 niligombea na jina langu lilikatwa na kamati ya uchaguzi ya TFF.Nilikata rufaa katika
Kamati ya Rufaa ya TFF na kushinda . Hukumu hii ni halali hadi leo.Iweje leo
hii miaka minne baadae Kamati hiyo hiyo ya rufaa (kubadili majina ya wajumbe
sio kubadili taasisi) inione sina uzoefu?.Si hilo tu ,hata katika kujaza fomu
namba moja ya kugombea niliambatanisha vielelezo vyote vya uzoefu wangu ikiwa
ni pamoja na kudhibitisha kuwa katika kipindi cha miaka mine iliyopita nimekuwa:
-Mjumbe wa Baraza la
michezo mkoa wa Dar es salaam.
-Mwenyekiti wa kamati ya
mashindano chama cha mpira mkoa wa Pwani COREFA.
-Mjumbe wa mkutano mkuu wa
mkoa wa Kagera
-Mwenyekiti wa chama cha
mpira mkoa wa Kagera
Hii ni pamoja na kuongoza
Yanga 2002-2005.
Hivi katika nafasi hizi za
uongozi ipi ni ya kuongoza ‘bonanza’? Nimedhalilishwa sana.
HITIMISHO
Vyombo vya habari kupitia
makala,tahariri na maoni ya wasikilizaji/wasomaji/watazamaji vimesifia sana
awamu mbili za uongozi wa Bwana Leodeger Tenga.Bwana Tenga amesifiwa kwa
umahiri wake wa kuleta utulivu katika sekta ya mpira wa miguu
Tanzania.Amesifiwa kwa kujenga taasisi imara ambayo mhimili wake mkuu ni
sekretarieti makini na kamati mbali mbali zilizo imara .Let him rise to the
occasion,muda wa kuonyesha uongozi imara ni huu,historia itamhukumu kwa jinsi
gani atasimamia suala hili,haki sio lazima itendeke lakini pia inatakiwa
ionekane inatendeka.
Kamati ya utendaji ya TFF
inayo mamlaka ya kubatilisha maamuzi haya kwa maslahi ya mpira wa
Tanzania.Ninamshauri Rais wa TFF aitishe kikao cha dharura cha kamati ya
utendaji ili kijadili hali hii na kunirudishia haki yangu ya kugombea urais wa
TFF.
Nihitimishe kwa kuwaomba
wadau wa mpira wa miguu Tanzania wawe
watulivu wakati tukisubiri kupata ufumbuzi wa suala hili.
Mungu ibariki Afrika,
Mungu ibariki Tanzania.
Ahsanteni sana,
Jamal Emil Malinzi
Dar es salaam
13/02/2013

No comments:
Post a Comment