MWENYEKITI wa CCM, Rais Jakaya Kikwete ameamua kuwatosa vinara
wanaotajwa kutaka kuwania urais kupitia chama hicho kutoingia kwenye
Kamati Kuu (CC). Dalili za kuwatosa vinara wanaotajwa kuwania urais
2015, ni kutokana na hatua yake ya juzi kuamua kutowapendekeza kuwa
miongoni mwa majina ambayo yangepigiwa kura ili kuweza kuingia katika
CC.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa ndani na nje
ya CCM wanaona hatua ya Kikwete kutopendekeza majina ya wanasiasa vigogo
wanaotaka urais 2015 kupitia chama hicho katika orodha ya watu 42 ili
kuwania nafasi 14 za CC kama mkakati maalumu wa kuwaweka kando.
Hata hivyo, mkakati huu wa Kikwete ulikuwa
hatua muhimu kwake kama kiongozi wa chama baada ya kukwama kuzuia
makundi kung’ara katika chaguzi zilizopita ambapo wafuasi wa Edward
Lowassa waliibuka kidedea kuanzia katika NEC, mikoani na Jumuiya za
chama hicho.
Ndiyo maana baada ya kumalizika Uchaguzi wa
wajumbe wa NEC, Kikwete alisita kuunda CC kwa maelezo kwamba
waliochaguliwa walikuwa wageni na alikuwa hawafamu vizuri. Hatua hii ya
Kikwete ilitafsiriwa kama mkakati wa kuzima nguvu ya mojawapo ya kambi. Hata
hivyo, kuna mtazamo tofauti kwamba hatua ya Kikwete kutopendekeza
majina makubwa na yenye nguvu ndani ya CCM kuwania ujumbe wa Kamati Kuu
inaweza ikawa ni njia ya kuwafanya wajumbe wa CC kuwa na kazi moja tu
ambayo ni kuchuja majina ya wagombea badala ya wao pia kuwa washiriki.
Kutoswa kwa vigogo Katika hali iliyozua
gumzo, majina ya wanasiasa vigogo Edward Lowassa, Benard Membe na Samuel
Sitta ha yakuwamo katika orodha ya Rais Kikwete aliyowasilisha mbele ya
NEC ili kupata wajumbe wa CC, ambacho ni chombo muhimu cha uamuzi ndani
ya chama hicho.
Lowassa, Membe na Sitta ndiyo wanaelezewa kuwa
na makundi makubwa yana yowaunga mkono kiasi cha kutishia uhai wa chama
hicho katika chaguzi zijazo. Makundi ya watu hao yamekuwa hasimu
kiasi cha wakati fulani, Kikwete kulazimika kuunda kamati ya watu watatu
chini ya Rais Mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, Makamu Mwenyekiti wa zamani
wa chama hicho, Pius Msekwa na Abdulrahman Kinana, ambaye ni Katibu Mkuu
wa chama hicho kwa sasa ili kusuluhisha mgogoro huo.
Hata hivyo, kansa ya mgogoro imeendelea na
kujipambanua waziwazi na hasa wakati wa Uchaguzi Mkuu wa chama hicho
mwaka jana wakati makundi hayo yalipopambana kujaza wafuasi wao kwenye
NEC kwa lengo la kujipanga kwa ajili ya uchagzui wa 2015.
Wafuatiliaji wa siasa za CCM wanaamini
kukosekana kwa Lowassa, Membe na Sitta bila shaka ni pigo kwa mbio za
wanasiasa hao kutaka kuingia Ikulu mwaka 2015. Kwani kama watapenya
kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais kupitia CCM mwaka 2015 watakuwa
wamefuata nyayo za Benjamin Mkapa ambaye aliteuliwa kugombea urais akiwa
si mjumbe wa CC.
Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Kikwete walikuwa wajumbe wa CC kabla ya uteuzi wao kugombea urais.
Maoni ya watu mbalimbali Baada ya CCM
kuhitimisha safu yake ya uongozi kwa Halmashauri Kuu ya chama hicho
(NEC) kuchagua wajumbe CC huku kikiwatosa wanaotajwa kutaka kuwania
urais 2015, baadhi ya wasomi wamesema kitendo hicho kinaonyesha kuwa
chama hicho tawala kimedhamiria kujiimarisha.
Wakitoa maoni kwa nyakati tofauti wasomi hao
walisema hali ingekuwa mbaya ndani ya chama hicho kama baadhi ya watu
hao wangechaguliwa kuwa wajumbe wa CC.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu Dar es Salaam, Profesa
Gaudence Mpangala alisema kutopendekezwa kwa Lowassa, Membe na Sitta
kulitarajiwa kwa kuwa viongozi wengi wa chama hicho walikuwa hawapendi
jinsi baadhi ya wanachama wa CCM wanavyoonyesha wazi dhamira yao ya
kuutaka urais. Mwananchi.
|
No comments:
Post a Comment