SAKATA la gesi limetua rasmi bungeni baada ya Kiongozi wa Kambi
ya Upinzani, Freeman Mbowe kuitaka Serikali iweke hadharani mikataba ya
utengenezaji wa bomba la kusafirishia gesi hiyo kutoka Mtwara kwenda Dar
es Salaam ili kuondoa usiri uliogubika mradi huo. Mbowe alitoa wito
huo jana alipokuwa akimuuliza Waziri Mkuu, Mizengo Pinda maswali bungeni
katika kipindi cha Maswali na Majibu kwa Waziri Mkuu.
“Mheshimiwa Waziri ni dhahiri kuwa vurugu
za Lindi na Mtwara zimesababishwa na mawasiliano hafifu kati ya Serikali
na wananchi, ikiwamo kauli za viongozi wa Serikali na CCM je, ni kwa
nini Serikali isiwachukulie hatua za uwajibikaji watumishi wa Serikali
na vyombo vya ulinzi na usalama ambao wanaonekana dhahiri kuhusika,”
alihoji Mbowe.
Kiongozi huyo wa upinzani alimtaka Waziri Mkuu
kueleza ni kwa nini Serikali isiweke wazi mikataba yote ya gesi ili
kuondoa hofu iliyojengeka kwa wananchi kwamba kumekuwa na hali ya
ufisadi.
Akijibu swali hilo, Pinda aliwataka wabunge
kutumia utaratibu mzuri wa kupata mikataba hiyo akisema haiwezekani
ikawekwa hadharani.
Mbali na jibu hilo, Pinda alivitupia lawama
vyama vya siasa akisema vimechangia kwa kiasi kikubwa mgogoro wa gesi
mkoani Mtwara.
Licha ya juzi kueleza kuwa kulikuwa na
mgogoro wa viongozi ndani ya mkoa huo pamoja na CCM, jana alikwepa swali
la kutaka wahusika wawajibike na badala yake akasema suala hilo liko
juu yake.
Alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali lingine
la Mbowe ambaye alimtaka Pinda kutoa kauli juu ya nani aliyesababisha
mgogoro wa Mtwara uliosababisha maafa.
Hata hivyo, alitangaza neema kwa waathirika
kwamba Serikali inaangalia namna ya kuwapunguzia gharama wale wote
waliopatwa na matatizo hayo ikiwamo kuwalipa fidia. “Vyama vya siasa
vimechangia kwa kiasi kikubwa katika kupotosha jambo hilo, ushindani wa
chaguzi zinazokuja umejitokeza pia,” alijibu Pinda.
Kiongozi huyo alisema wanaofanya uchochezi huo
wanafanya bila ya kujua kwamba unaweza kuwakumba watu wote wakiwamo hao
wanaofanya hivyo. “Tutalaumiana wengi lakini ni vyema kuweka mambo
hadharani na kwamba ni hatari kufanya mambo kama hayo kwani amani ya
nchi ni lulu ambayo ikipotea inaweza kuwa tabu kuipata.”
Alipinga hoja ya Mbowe kuwa Serikali
inatekeleza majukumu yake baada ya shinikizo na maandamano ya wanasiasa.
Alilieleza Bunge kuwa wananchi wa Mtwara wanaweza
kupoteza fursa nyingi kutokana na wawekezaji kuanza kuondoka wakikwepa
vurugu na kukimbilia Msumbiji ambako kuna dalili za gesi pia.
Kamati ya Makinda yayeyuka Jana, Spika wa
Bunge Anne Makinda aliliambia Bunge kuwa Kamati aliyotarajia kuiunda
haitakuwapo kutokana na ukweli waliokuwa wakiutaka kutoka Mtwara
kuelezwa na Waziri Mkuu.Mwananchi. |
No comments:
Post a Comment