![]() |
| Kalonzo Musyoka. |
MGOMBEA mwenza wa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga, amesema kuwa kuna
ushahidi kuonyesha kuwa kuna hujuma dhidi yao katika dhughuli ya kuhesabu kura
inayoendelea katika ukumbi wa Bomas, na kwamba shughuli hiyo inastahili
kusitishwa.
Hata hivyo alisema kuwa haina maana kuwa
wanaitisha maandamano.
Shughuli ya kuhesabu kura ingali
inaendelea ingawa kwa mwendo wa kinyonga baada ya tume hiyo kutupilia mbali
mitambo yake ya kuhesabu kura baada ya kugoma. Uhuru Kenyatta angali anaongoza
kwa idadi ya kura za wagombea wa urais akiwa na kura 2,660,379 dhidi ya
mpinzani wake Raila Odinga aliye na kura 1,996,181 lakini matokeo rasmi
yatajulikana tu mwishoni mwa juma.
Taharuki imetanda na kuna hali ya
wasiwasi kwani tume ya uchaguzi haijatangaza matokeo ya urais zaidi ya masaa
arobaini na nane tangu wakenya kupiga kura. Muungano wa CORD umesema kuwa
unatafakari hatua za kuchukua baada ya kudai hujuma katika shughuli
inayoendelea ya kuhesabu kura za urais.
Shughuli hiyo imekumbwa na utata hasa
baada ya mitambo ya kuhesabu kura ya tume ya uchaguzi kukumbwa na hitilafu. Hatua
hii imelazimu tume hiyo kuanza kuhesabu kura upya katika kitovu cha kupokea
matokeo ya kura za urais kwenye ukumbi wa Bomas viungani wa mji wa Nairobi.
Kalonzo Musyoka ambaye ni mgombea mwenza
wa Raila Odinga, amehutubia waandishi wa habari mjini Nairobi na kusema kuwa
muungano wa CORD, unataka shughuli hiyo ya kuhesabu kura za urais kusitishwa
mara moja na kuanzishwa upya wakitumia stakabadhi kutoka kwa makarani wa kura
jambao ambalo linafanywa kwa sasa
Musyoka vile vile amesema kuwa muungano
huo una tashwishi kuhusu baadhi ya matokeo wakisema sio ya kweli kwa kuwa
hayawiani na yale waliyoyaleta maajenti wao. Aliendelea kwa kusema kuwa baadhi
ya matokeo yako juu kuliko idadi ya wapiga kura katika baadhi ya maeneo ambako
kura zilipigwa.
Musyoka amesisitiza kuwa tatizo hilo
limetokana na kugoma kwa mitambo ya kupiga kura na pia kuanza upya kwa shughuli
ya kuhesabu kura kwa kutumia mfumo wa zamani.
Musyoka alisema kuwa tume ya uchaguzi
inastahili kutumia mitambo ya elektroniki kuhesabu kura kama inavyoagiza katiba
ya nnchi, huku akiongeza kuwa muungano huo ungali unatafakari hatua za kuchukua
ingawa kwa kufuata sheria. Moja ya hatua inazotafakari kuchukua ni kwenda
mahakamani kuitaka mahakama kusimamisha shughuli ya kuhesabu kura na kuanza
tena.


No comments:
Post a Comment