![]() |
Rais wa Marekani Barack Obama akiwasalimia wasanii wa nchini Senegal juzi alipotembelea kisiwa cha Goree, kilichopo pwani mjini Dakar alipokuwa ziarani nchini humo. |
Dar es Salaam.
Wakati magari 150 ya msafara wa ziara ya Rais Barack Obama yamewasili nchini, majina ya mawaziri wa Tanzania yatakayoruhusiwa kumpokea kiongozi huyo kuchujwa na makachero wa FBI.
Wakati magari 150 ya msafara wa ziara ya Rais Barack Obama yamewasili nchini, majina ya mawaziri wa Tanzania yatakayoruhusiwa kumpokea kiongozi huyo kuchujwa na makachero wa FBI.
Mkurugenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mwalimu Julius
Nyerere, Moses Malaki aliliambia gazeti hili jana kuwa matayarisho ya
ujio wa Rais huyo ni kabambe na hayajawahi kutokea katika historia ya
Tanzania.
Pia alisema shughuli za kumpokea Rais Obama,
anayetarajiwa kutua Jumatatu saa 8:40 mchana, zitaanza asubuhi kwa
maofisa wa Marekani kushika majukumu yote katika uwanja huo, ikiwemo
kuongoza ndege, ukaguzi wa abiria na mizigo, kwa maana wafanyakazi wa
uwanja huo kuwa likizo kwa siku mbili.
“Wamesema kuwa wao watasimamia kila kitu kuanzia
wageni watakaoingia na kutoka na wataamua nani aingie na kutoka,”
alisema Malaki.
Aliongeza kuwa japokuwa Mamlaka ya Anga Tanzania
(TAA) inaendelea kufanya kazi zake kama kawaida, lakini Jumatatu,
Wamarekani watasimamia kila kitu hadi ukaguzi wa wageni.
“Siku hiyo mwongoza ndege wa TAA, atafanya shughuli kidogo, mambo mengine yatafanywa na wao,” alisema.
Idadi ya maofisa wa Tanzania
Imebainika kuwa hata idadi ya maofisa wa Tanzania wakiwemo viongozi watakaompokea pia itapangwa na Wamarekani wenyewe.
“Wenyewe wana orodha yao na wanajua nani atakuwepo
au hatakiwi kuwepo katika kundi la wageni watakaompokea Rais Obama,”
alisema na kuongeza:
“Nilimuuliza Ofisa Usalama wa Marekani iwapo
nitaweza kumwona Rais Obama, akaniambia: Utamwona ukibahatika kuwepo
kwenye orodha.”
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe naye
alikiri kuwa mawaziri wanaotakiwa kuwepo katika msafara wa kumpokea Rais
Obama ni wachache watakaochaguliwa tu na Wamarekani, baada ya kuyapitia
na kuyachunguza majina hayo kwanza kabla ya kuyakubali.
“Hii sijawahi kuiona, hata sisi wenyewe tunateuliwa na wakishayapitia wataamua, nani aende au asiende,” alisema Chikawe.
Malaki anaendelea kueleza kuwa maofisa usalama kutoka Marekani
wamekuwa wakifanyia ukaguzi kila eneo la uwanja huo, kwa kiwango cha
hali ya juu na kinachoshangaza.
Ilibainika kuwa maofisa hao wameagiza hata miti
mirefu na yenye matawi mengi ikatwe ili kuondoa nafasi ya adui kufanya
mashambulizi.
“Hawa jamaa hawataki kufanya makosa, kitu chochote wanachokitilia shaka wanakiondoa na kukisimamia ipasavyo,” alisema.
Malaki alisema licha ya maofisa hao kuambiwa kuwa
miti hiyo mikubwa ipo katika ofisi za Jeshi la Polisi wa uwanja wa
ndege, walikataa kata kata na kuagiza ifyekwe.
Mafuta ya ndege
Katika kuhakikisha kuwa hakuna chochote cha hatari
kinachoweza kuipata ndege ya Rais Obama, maofisa hao wamenunua mapipa
kumi ya mafuta ya ndege na kuyahifadhi katika eneo nyeti la uwanja huo.
“Wamenunua mafuta na kuyahifadhi wao wenyewe na kuyafanyia vipimo vya hali ya juu,” alisema.
Huduma za zimamoto hazihitajiki
Wakati huduma ya zimamoto ikiwa inahitajika zaidi
wakati ndege inapotua au kupaa, maofisa wa usalama wa Marekani wamekataa
kutumia zimamoto wa Tanzania.
“Katika maandalizi hayo, tulitaka kuandaa gari la
zimamoto ambalo kwa kawaida linatakiwa liwepo ndege inapotua, lakini
walisema halina haja siku hiyo,” alisema Malaki.
Aliongeza kuwa maofisa hao hawaamini mtu yeyote
ikiwamo wafanyakazi wa Jeshi la Zimamoto katika kumpokea Rais Obama,
hasa wakati atakapokuwa anatua.
Wakati huohuo, gari lililobeba maofisa usalama wa Marekani
likiongozwa na pikipiki ya askari wa usalama barabarani ambalo
lilionekana likizunguka katika barabara kuu za jiji katika kile
kilichobainika ni kuhakiki usalama wa barabara hizo.
Shughuli za usafi ndani ya uwanja huo zimeendelea
kufanyika, ambapo Malaki amekiri kupewa agizo na Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Said Meck Sadick kufanya usafi katika viwanja vyote vya ndege.
Kamanda wa Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Suleiman Kova, alisema wakati huu wa ujio wa Obama, ulinzi ni mkali na
wa kutisha kwa wahalifu na wa kufurahisha kwa raia wema.
“Ofisi haikaliki, hapa nilipo nipo doria nahakikisha kila kitu kinakwenda sawa, hatutaki kufanya makosa,” alisema Kamanda Kova.
Alisema mtandao mkubwa wa askari umeshawekwa
tayari barabarani kuhakikisha kila kitu kinakwenda kama ilivyopangwa
hadi siku ya tukio lenyewe.
Mfanyakazi wa uwanja huo, William Masuka, alisema
hali katika uwanja huo imebadilika na uwanja umefurika maofisa usalama
wa Marekani ambao wanakagua kila eneo.
“Hawa watu wamefurika hapa, sijawahi kuona kabisa. Wapo kila mahali na wapo makini,” alisema William.
Masuka alisema ulinzi wa eneo hilo hauwezi kufananishwa na ziara yeyote ya marais wakubwa waliowahi kufika hapa.
Magari 150 yatua Dar
Taarifa za uhakika zinaeleza kuwa ndege hizo
zilitua jana saa 5:00 usiku, zikiwa na uwezo wa kubeba magari zaidi ya
50 kila moja. “Hii ni historia, wamekuja marais wengi hapa, lakini
ukaguzi, ulinzi na matayarisho mengine kama haya hayajawahi kutokea,”
alisema Malaki.
Alisema hivi sasa mazoezi ya kumpokea Rais huyo
uwanjani hapo yanafanyika ambapo bendi rasmi ya askari wa Tanzania
itakayotumbuiza siku hiyo, maofisa wa Marekani na viongozi wa TAA,
wanafanya mazoezi na kuelekezana jinsi watakavyompokea Rais Obama.
“Mazoezi haya yatatoa picha rasmi ya jinsi Rais
huyo atakavyotua, wapi bendi ikae, wapi maofisa wasimame, wapokeaji na
msafara wake mzima.
No comments:
Post a Comment