- Bismillahi ‘Aliyyun, Ya Ilahi Ya Rahimu
Bismillahi Qawiyyun, nguvu ni Zako Qayyumu
Bismillahi Ghafurun, toba ni Kwako Hakimu
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Bismillahi Basirun, unatuona wajao
Bismillahi Samiun, tusikize viumbeo
Bismillahi Munirun, nawirisha wakuchao
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia - Rehema Zako Rabana, zeleya kila mahala
Rehema za Subhana, zenda kwa hata kabwela
Rehema za Maulana, kwa ‘asi na mcha Mola
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Awali ya Ramadhani, kumi limejaa heba
Kwa kusoma Qur’ani, na kukithirisha toba
Wokovu kwa waumini, Rabbi utupe haiba
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Tufunge tukihimidi, rehema zako Rabbana
Tufunge tukikunadi, turehemu Ewe Bwana
Tufunge tukiburudi, Amina Rabbi Amina
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Tukitaja jina Lako, tuburudike nafusi
Tukiona waja Wako, tukukumbuke Mkwasi
Tukiwa na Peke Yako, tujiepushe kuasi
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Tukwogope hadharani, na zaidi faraghani
Kubali wetu ugeni, Ilahi Ya Rahmani
Bila ya Kwako Manani, twende kwa mwengine nani?
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia. - Takabali zetu dua, saumu na sala pia
Waja tumejaa doa, pumzi zinafifia
Hatutendi kwa kujua, Ya Rabbi twakulilia
Heko kumi la rehema, Allah katujaalia.

No comments:
Post a Comment