ABBAS MAZIKU BUNDALA, Mtanzania wa kwanza kufanya biashara ya korosho nchini Vietnam - RAHA ZA PWANI

Habari za Hivi Punde

Responsive Ads Here

Post Top Ad

Post Top Ad

Responsive Ads Here

Tuesday, August 25, 2015

ABBAS MAZIKU BUNDALA, Mtanzania wa kwanza kufanya biashara ya korosho nchini Vietnam

Mfanyabiashara wa kimataifa  anayejihusisha na biashara ya mazao, Abbas Maziku akifafanua  jambo katika mahojiano na Tanzania Daima kuielezea shauku yake ya kutaka kuwa mfanyabiashara mkubwa kama Mohammed Dewji(Mo).
Abbas Maziku akiwa katika moja ya shughuli zake za kusafirisha mazao kuelekea mataifa mbalimbali katika Bandari ya Mtwara  kama makontena yaliyohifadhiwa  mazao hayo yanavyoonekana  nyuma yake.
Mfanyabiashara wa kimataifa, Abbas Maziku akiwa ofisini kwake  maeneo ya Posta Mpya jijini Dar es Salaam.
Mfanyabiashara wa kimataifa,  Abbas Maziku akiwa na  mfanyabiashara tajiri na mwenye umri mdogo anayemiliki Kampuni ya Mohammed Interprises(MeTl)Mo Dewji.
Magunia ya korosho  yakisubiri kupakiwa kwenye makontena tayari kwa kusafirishwa kwenda  nchini Vietnam ambapo mfanyabiashara, Abbas Maziku hufanya nao biashara kwa mkataba maalumu.
NA  MWANDISHI WETU

BIASHARA ya kusafirisha mazao ina ushindani mkubwa kutokana na kutawaliwa na matajiri wenye asili ya Kiasia.
Sababu hiyo imewafanya Waafrika wengi kutokuwa na uthubutu katika biashara hiyo kwa kuhofia kutofanikiwa na kujitanua kibiashara.
Mbali na ugumu huo lakini pia wengi hasa Watanzania wamejikuta wakiishia kuwa wafanyabiashara wa kawaida na kupoteza fursa za kimataifa.
Kupoteza fursa muhimu za kimataifa kumefanya wakose nafasi ambazo zingeweza kuwafanya kufikiri nje ya boksi.
Makala hii inamwangazia mfanyabiashara wa kwanza wa Kitanzania kufanya biashara ya kusafirisha korosho kwenda nchini Vietnam, Abbas Maziku.

Alipoanzia

Maziku anasema alianza biashara ya kusafirisha mazao mnamo mwaka 2013 baada ya kuvutiwa na mjomba yake ambaye alikuwa na mashamba yaliyokuwa na mazao mbalimbali.

Miongoni mwa mazao  ambayo Maziku alianza nayo na anaendelea nayo ni korosho, ufuta, mbaazi, choroko, mtama, alizeti, mashudu ya pamba  na pilipili Manga.
Anasema mazao hayo huyakusanya kutoka kwa wafanyabiashara wadogo wadogo, wakulima pamoja na kwenye minada  inayofanywa na vyama vya ushirika katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Dodoma, Singida, Shinyanga na Tanga.

Anayasafirisha kwa njia gani?

Akizungumzia jinsi anavyosafirisha mazao hayo, Maziku anasema hutumia gari kuyatoa mikoani hadi kuyafikisha maghalani na kuyahifadhi kabla ya kufungasha.
“Wakati wa kuyafungasha unapofika huwa nayafungasha  kwa kutumia vibarua na katika vifungashio vyangu huwa na nembo  inayoonyesha jina la kampuni yangu  na baada ya hapo sampuli hupelekwa katika maabara za kupima ubora wa mazao kimataifa iitwayo SGS  na ndipo hufuatiwa na hatua ya mwisho ya usafirishaji  ambayo huwa natumia meli za mashirika mbalimbali ikiwamo IPTL, MAERSK  na nyinginezo kwa ajili ya kwenda nchini Vietnam,” anasema  Maziku.
Anabainisha baada ya hatua zote hizo hufuata taratibu zinazotakiwa ikiwemo kulipia ushuru kwa Mamlaka ya mapato nchini, (TRA), wataalamu kutoka Wizara ya Kilimo na ufugaji, wanasheria pamoja na maofisa wa Usalama wa Taifa ambao huhakikisha hatua zote halali zimefuatwa.

 Maziku anasema kwamba kwa biashara za kimataifa Shirika la Viwango (TBS) na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA)  hawahusiki bali wahusika wakuu ni SGS.
 
Anajiendeshaje kibiashara?

Maziku anajinasibu kwamba biashara ya kuuza mazao nje ya nchi ina ushindani mkubwa.
Anasema anakumbuka alianza na mtaji wa sh. 2,000,000 na sasa anazungumzia mtaji wa sh. milioni 200.
 “Si rahisi kufika nilipofikia  kwasababu biashara hii ina  ushindani mkubwa, ninashindani na matajiri wakubwa wenye uwezo wa kujipangia bei za mazao hivyo ingawa nimepiga hatua lakini bado ninahitaji kupanua biashara yangu zaidi na zaidi”anasisitiza .
Anaeleza kwamba mwaka 2013 alipata hasara ya baada ya ubora wa mazao aliyopeleka kupimwa na kuonekana upo kwenye kiwango cha 48 badala ya 51 inayotakiwa hivyo ilimpa wakati mgumu na kuyumba  kibiashara na  mtaji wake kukata ndipo alipolazimika kukopa fedha benki ambapo hadi sasa  bado analipa deni hilo.
“Nilipata hasara kubwa sana ambayo hadi leo hii bado ninalipa hilo deni nililokopa benki  ingawa pia fedha kutoka kwenye vyanzo  mbalimbali vya mapato ya biashara zingine ninazozifanya zinaendelea kuifanya bishahara ya mazao kwenda nje ya nchi iendelee kuwepo,” anasema.

Vikwazo vya kibiashara

Maziku anakwenda mbali na kueleza katika jambo lolote lenye mafanikio vikwazo huwa havikosekani lakini kubwa katika ni mtaji.

Pia analia na ukiritimba unaofanywa na benki mbalimbali ambao hutaka dhamana kubwa kuliko uwezo wa mfanyabiashara.
Ukiachilia mbali suala la benki, Maziku anasema kikwazo kingine ni ukiritimba kwenye vyama vya ushirika  katika suala zima la upangaji wa bei ambazo hukinzana na bei ya katika soko la dunia hivyo inakuwa ngumu kwa wafanyabiasahara kufikia malengo kutokana na kuepuka kupata hasara.
Aidha, anataja vikwazo vingine ni wizi wa fedha unaofanywa na baadhi ya watu anaowaamini kumnunulia mazao ambao  hutoroka na fedha hivyo kufanya suala la uaminifu kuwa mdogo na vikwazo vya ubora wa mazao.

Mafanikio

Akizungumzia mafanikio Maziku anabainisha, tangu alipoanza biashara ameweza kuwa na kampuni mbili zijulikazo kama Agromart Company Limited (GEFU) na Lyone Investment Company Limited  ambazo kwa pamoja ameajiri wafanyakazi watano akiwemo Ofisa Rasilimali Watu, Mhasibu, katibu Muhtasi, Mwanasheria na Meneja Mwendeshaji wa shughuli za kampuni.
Anaeleza kwa biashara anayoifanya ameweza kujenga nyumba yake mwenyewe, kumiliki usafiri na kupata fursa za kusafiri nchi mbalimbali kuhudhuria makongamano na maonyesho ya biashara ya mazao jambo ambalo limemkutanisha na watu na kupanua wigo wa biashara yake kimataifa.
Maziku anasema anatarajia kufungua kampuni ya ujenzi ili mtaji wake uzunguke pamoja na kutoa ajira kwa vijana mbalimbali wa Kitanzania.

Matarajio mengine ni kuanzisha  kiwanda cha uzalishaji wa bidhaa  ndogo ndogo za majumbani kama vile juisi, mafuta ya alizeti, mifuko ya plasitik pamoja na maji ya kunywa kwa ushirikiano na wawekezaji kutoka nje kwa lengo moja tu la kukuza uchumi wa Tanzania.
Aida anasema anajihusisha kikamilifu na masuala ya kijamii hasa kusaidia wasiojiweza ikiwemo yatima lakini mambo hayo huyafanya nyuma ya pazia pasipo kujitangaza.
“Kidogo nilicho nacho huwa nakitoa kwa wenye mahitaji maalum lakini huwa sijitangazi” anasema. 
Maziku ni kijana wa Kitanzania aliyezaliwa mwaka 1990, kitaaluma yeye ni mtaalamu wa masuala ya benki na fedha  fani ambayo alisoma katika chuo kikuu cha Zanzibar.
 Pia aliwahi kufanya kazi Benki ya Exim kama ofisa wa kawaida wa benki ambayo alidumu nayo kabla ya kugeukia katika biashara ya mazao.
Maziku ni mtoto wa mwisho kwenye familia yao yenye watoto watatu, ndoto yake ni kuwa mfanyabiashara mdogo mwenye mafanikio makubwa kama alivyo Mohammed Dewji(Mo).
Aidha Maziku anawashauri vijana wenzake wawe na uthubutu kama aliokuwa nao yeye, aliiona fursa kaichangamkia.
“Vijana tusibweteke,vikwazo ni vingi,hatupaswi kukata tamaa, hata waliofanikiwa kama  akina Mo hawakuanzia juu, walipambana  na uzuri ni kwamba Mo si mchoyo, ni mtu anayejitoa, mwenye msaada katika mambo mbalimbali ya ushauri wa kibiashara jambo ambalo linanifanya nimuheshimu na amechangia  katika mafanikio yangu ya kibiashara hivyo sitaacha kumshukuru,” anasema.

Aidha Maziku anamshukuru rais  Jakaya Kikwete  kwa kuwa miongoni mwa watu waliochangia mafanikio yake.
0658 266 406
Chanzo :Tanzania Daima Gazeti,August 25,2015
MWISHO

1 comment:

Post Top Ad

Responsive Ads Here